• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
LIKIZO: Wito watoto wanaoenda kuogelea baharini wasajiliwe

LIKIZO: Wito watoto wanaoenda kuogelea baharini wasajiliwe

Na KALUME KAZUNGU

WITO umetolewa kwa serikali ya kaunti ya Lamu kuunda sheria itakayohakikisha watoto wote wanaozuru fuo za bahari eneo hilo kuogelea wanasajiliwa.

Hii ni kufuatia ongezeko la visa vya watu kufa maji wakiogelea kwenye sehemu mbalimbali za ufuo wa Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu.

Katika kikao na wanahabari Jumapili, wanachama wa Muungano wa Wanawake eneo hilo, walieleza haja ya kaunti kurekodi watoto wote ambao watakuwa wakizuru kwenye fuo za Lamu hasa msimu huu wa likizo ndefu kwa shughuli za uogeleaji.

Walisema hatua hiyo itasaidia kuzuia matukio ambapo watoto huishia kutoweka baharini wakati wakipogelea bila kugunduliwa waliko.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wanawake enepo hilo, Bi Fatma Salim, alisema idadi ya watoto wanaoogelea kwenye fuo za bahari mjini Lamu, Shela, Mkokoni, Kizingitini, Faza, Kiwayu, Ndau na visiwa vingine imeongezeka pakubwa hasa tangu shule zilipofungwa takriban majuma mawili yaliyopita.

“Kaunti ianzishe mpango wa kuwasajili watoto wa hapa Lamu na hata wale wa kutoka kaunti zingine wanaozuru Lamu kujivinjari kupitia uogeleaji kwenye fuo zetu za bahari hasa msimu huu wa likizo. Wasiwasi wetu ni kwamba huenda watoto waangamie baharini bila ya hata kutambulika walikokuwa wakiendeleza uogeleaji. Kupitia usajili, mambo yatakuwa rahisi kinyume na ilivyo sasa,” akasema Bi Salim.

Naye Bi Halima Bwanamkuu aliwataka wazazi hasa kwenye ukanda wa Pwani kuhakikisha watoto wao wanapokea mafunzo ya uogeleaji kabla ya kuwaruhusu kutekeleza shughuli hiyo baharini wenyewe.

Bi Bwanamkuu pia alisisitiza haja ya wazazi kufuatilia kwa karibu shughuli za watoto wao baharini ili kuepuka kuwapoteza watoto hao.

“Wakati umewadia kwa wazazi wenyewe kuwapokeza watoto mafunzo ya kimsingi yanayohusu uogeleaji. Si vyema mtoto kumuacha kwenda baharini kuogelea licha ya kwamba hana ufahamu wowote kuhusu shughuli hiyo,” akasema Bi Bwanamkuu.

Muungano huo wa Wanawake wa Lamu pia uliiomba kaunti kubuni kitengo maalum cha kukabiliana na majanga ya baharini punde yanapotokea.

Walisema inashangaza kwamba eneo la Lamu ambalo usafiri wake hutegemea sana bahari halina miundomsingi yoyote ya kukabiliana na majanga ya baharini.

“Wabuni vikosi maalum vitakavyokuwa vikipiga doria kwenye fuo za bahari kote Lamu ili kuokoa wal;e wanaoogelea, kutekeleza uvuvi au kusafiri baharini ambao huenda wakakumbana na mikosi na kulemewa na mawimbi mazito baharini,” akasema Bi Asha Habib.

Kauli ya akina mama hao inajiri siku mbili baada ya mwanamume wa makamo kufa maji ilhali mwingine akiokolewa na wapigambizi wa kujitolea wakati wakiogelea katika eneo la Shela, Kaunti ya Lamu.

You can share this post!

Mitandao lawamani kwa mimba za mapema

TAVETA: Wagonjwa wa saratani kupata afueni katika kituo...

adminleo