• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
Msichana akatalia kituoni hadi mvulana mpenziwe aachiliwe huru

Msichana akatalia kituoni hadi mvulana mpenziwe aachiliwe huru

Na STEPHEN ODUOR

MSICHANA wa miaka 17 katika Kaunti ya Tana River, amekataa kuondoka katika kituo cha polisi alipoachiliwa huru baada ya kukamatwa, akisisitiza lazima mwanamume anayedai kuwa ni mpenzi wake aachiliwe kwanza.

Msichana huyo alikamatwa pamoja na mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 29 katika ufuo wa bahari wa Bamburi, Kaunti ya Mombasa, baada ya mamake kupiga ripoti kwamba alikuwa amepotea.

Mamake alisema alimfahamu mwanamume huyo: “Nilimjua mwanamume huyo kwa muda kikazi. Alionekana kama mtu aliyejali maisha yangu na ya watoto wangu na alikuwa akitusaidia. Sikutarajia angeleta mashaka aina hii nyumbani kwangu.”

Mama huyo alieleza kuwa alifahamu tu kuhusu jinsi binti yake alivyokuwa akitoroka nyumbani usiku alipoambiwa na watoto wake wengine na alipomwadhibu akatoroka.

Alisema msichana huyo, ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alikuwa akitoka nyumbani kisiri na wanaume wawili ambao humchukua kwa gari.

Hayo yalikuwa yakifanyika wakati mamake akiwa kazini usiku, kisha anarejea alfajiri kabla mamake hajarudi nyumbani.

Mamake ndiye alifichua kuwa binti huyo alikataa kuondoka katika kituo cha polisi hadi mwanamume huyo aachiliwe huru na waruhusiwe kuoana.

Babake msichana huyo alisema alipoenda kituoni alimpata binti yake wakilishana chakula na mshukiwa huyo mbele ya polisi, huku akitoa madai ya kushtua kumhusu mamake.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Tana River, Bw Patrick Okeri, alithibitisha kisa hicho lakini akasema msichana huyo alidai mamake hana maadili mema na amekuwa akimtesa ndiposa hataki kurudi nyumbani.

Bw Okeri alisema msichana huyo alikanusha madai kwamba alipelekwa Mombasa na akasisitiza alienda mwenyewe kwani hangeweza kuishi na mamake aliyetaka kumgeuza kahaba.

“Hatuwezi kupuuza madai ya msichana huyo kwani ana alama ya jeraha ambalo hatuwezi kuthibitisha kama ni la kisu na uchunguzi wa kimatibabu pia haujathibitisha kuwa alinajisiwa,” akasema.

Alisema mwanamume huyo atapelekwa kortini ili mahakama iamue hatua inayopaswa kuchukuliwa, huku wakisubiri mwelekeo kutoka kwa idara ya watoto kuhusu kama msichana huyo atapelekwa kuishi makao salama.

You can share this post!

Hatimaye Mugo wa Wairimu abambwa

SHERIA ZA MICHUKI: Msako sasa waingia hongo

adminleo