• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Amerika yatumia wafungwa 4,000 kuzima moto California

Amerika yatumia wafungwa 4,000 kuzima moto California

PETER MBURU na MASHIRIKA

MOTO mkubwa ambao umekuwa ukiteketeza jimbo la California, nchini Marekani umeisukuma serikali ya nchi hiyo kuanza kuwatumia wafungwa kuuzima ili kupunguza hasara.

Shirika moja la habari kimataifa limeripoti kuwa serikali ya California inawatumia takriban wafungwa 4,000 kusaidia kazi za kuuzima moto huo ambao tayari umesababisha hasara ya mamilioni ya pesa, kuhamisha maelfu ya watu na kuua watu 44 hadi sasa.

Hata hivyo, sio kila mfungwa ana nafasi ya kushiriki kazi hiyo, ila ni wale tu ambao wamedhihirisha tabia na maadili mema wakati wakitumikia kifungo, nao kwa kazi hiyo wanatuzwa vilivyo.

Kwa mfano, japo kikawaida pesa nyingi ambazo mfungwa anaweza kulipwa kila siku katika jela za jimbo hilo ni $2.56, wale wanaofanya kazi ya kuzima moto wanalipwa dola moja kila saa ya kazi.

Vilevile, kila siku wanayofanya kazi hiyo inapunguza kifungo chao kwa siku mbili, jambo ambalo limefanya wafungwa kuunda asilimia kati ya 30 na 40 ya wafanyakazi ambao wanashiriki kuzima moto huo.

Hata hivyo, wafanyakazi ambao ni raia wa kawaida wanalipwa $17.70 kwa saa wanapozima moto huo.

Wafungwa wamekuwa wakitumiwa kung’arisha vichaka na kuchimba mashimo.

 Idara ya magereza California imetangaza kuwa kutokana na kuwatumia wafungwa, serikali imeokoa pesa za walipa ushuru zaidi ya $100milioni, suala ambalo limefanya watu wengi kushangaa ikiwa serikali ya jimbo hilo inaweza kukaa bila wafungwa wenye adabu njema, kwani wamekuwa wakisaidia katika majanga hayo hata siku za mbeleni.

Bw Travis Reader, mfungwa mmoja aliyekuwa akifanya kazi hiyo alisema anatumai kuwa kazi hiyo sasa itampa fursa ya kupata utaalamu ilia pate kazi wakati atakapoachiliwa huru.

“Kwa kweli ninataka kuwa na kazi ya kitaluma nitakapowachiliwa huru. Hii ni kwa ajili ya kurekebisha tabia na nilitaka kitu cha umuhimu kufanya na maisha yangu baada ya kifungo,” akasema Travis.

Hata hivyo, japo wamepokea mafunzo ya kutosha, wafungwa hao hawawezi kupata ajira katika idara hiyo kwani haiajiri watu wenye historia ya jinai.

Jimbo hilo la California limekuwa likikumbwa na visa vya mioto ya aina hiyo tangu miaka ya jadi na limekuwa na hulka ya kuwatumia wafungwa kusaidia kupunguza makali ya majanga hayo kwa gharama ya chini.

You can share this post!

Uongo aliotumia mama wa miaka 62 kupata mimba

Mwanamke afichua kuvuta bangi kila siku kulimsaidia...

adminleo