• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Maafisa wawili wa polisi kunyongwa

Maafisa wawili wa polisi kunyongwa

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wa polisi Jumatano walihukumiwa kunyongwa kwa kumuua mwenzao wa kitengo cha Utawala pamoja na jamaa zake wawili miaka minne iliyopita.

Jaji Stella Mutuku (pichani) aliamuru Koplo Benjamin Kahindi Changawa na Stanley Okoti wanyongwe kwa mujibu wa sheria kwa kuwua Konstebo Josephn Obongo Onchuru.

Usiku huo huo wa Oktoba 7 2014 , Jaji Mutuku alisema Koplo Changawa na Koplo Okoti waliwaua  jamaa wa afisa huyo wa polisi wa utawala Geoffrey Nyabuto Mogoi na Amos Okenye Makori.

Jaji Mutuku alisema kuwa maafisa hao wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kwa kuwamiminia risasi watatu hao bila sababu.

“Waathiriwa walikuwa wamejisalamisha. Onchuru alikuwa ameinua mikono na kujitambua kuwa alikuwa na bastola. Mogoi na Okenye walikuwa wamelala kwenye sakafu katika kilabu cha M-Club kilichoko mtaani Kangemi kaunti ya Nairobi,” alisema Jaji Mutuku.

Aliongeza kusema kuwa Onchuru hakuwatisha wala kutumia silaha aliyokuwa nayo aidha kwa maafisa hao wa polisi ama kwa wauzaji katika kilabu hicho ama kumtisha bawabu aliyepiga simu kusema kulikuwa na wezi wenye silaha kilabuni.

Koplp Changawa alikuwa amehudumia idara ya polisi kwa miaka 30 na Koplo Okoti alikuwa ametumikia kikosi cha polisi kwa muda wa miaka 20.

Akasema Jaji Mutuku akipitisha hukumu , “ Washtakiwa walikuwa wamehudumia kikosi cha polisi kwa miaka mingi. Walitumia mamlaka yao vibaya baada ya wahasiriwa kujisalamisha.”

Jaji alisema kitendo cha washtakiwa hao kilidhihirisha kuwa walikosa nidhamu na wanastahili kuadhibiwa vikali.

“Wawili hawa wanastahili adhabu kali na adhabu hiyo ni kifo,” alisema Jaji Mutuku akitamatisha akisema , “ mtanyongwa kwa njia iliyotangazwa kisheria.”

Alipitisha adhabu ya kifo kwa kosa la kumuua Onchuru na akasitisha adhabu kwa ajili ua Okenye na Makori hadi adhabu ya kwanza itekelezwe.

Onchuru alikuwa mlinzi wa Mbunge wa  Bomachoge Borabu Bw Joel Onyancha.

Alimsindikiza Bw Onyancha hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kisha akarudi katika kampi yao iliyoko mtaa wa Kitisuru na kuekeza gari la mwanasiasa huyo kisha akatoka na jamaa zake hao waliouawa pamoja naye.

Mahakama ilifahamishwa kuwa marehemu alirudi usiku na kuomba ruhusa msimamizi wa kampi hiyo aende kunua kadi ya simu.

Hata hivyo  yeye (Onchuru) na jamaa zake Mogoi na Okenye walienda kilabu kubugia kileo. Lakini Onchuru hakuwa analewa mbali alibarizi kwenye meza moja akiwa peke yake.

Muuzaji pombe kwenye kilabu hicho aliingiwa na hofu na kumweleza bawabu kuhusu Onchari.

Bawabu alimwendea Onchuru na kumtaka aeleze anachofanya kwenye kona ya jumba hilo la kuuzia pombe.

Badala ya kujibu Onchuru alitoa bastola na kumwelekezea askari huyo.

Hali ya mshike mshike ilizuka. Msimamizi wa kilabu hicho aliwaita maafisa wa polisi na kuwaambia wamevamiwa na wezi waliojihami na silaha.

Hata hivyo bawabu huyo na muuzaji pombe walimkamata Onchuru na kumfungia ndani ya stoo.

Washtakiwa walifahamishwa wajihadhari wanapoelekea kwenye kilabu kwa vile washukiwa wa ujambazi walikuwa wamejihami kwa bastola.

Mahakama ilijulishwa washtakiwa walikuwa wanatoka katika kituo cha polisi cha Kabete Special Lock Up.

Walipofika kwenye kilabu washtakiwa waliwaua Onchuru na jamaa wake wawili Nyabuto na Okenye.

Wakijitetea washtakiwa waliambia mahakama walijitambua kwa wahasiriwa kisha wakawataka wajisema wao ni kina nani lakini wakakaidi.

Ushahidi ulisema kuwa wateja wale wengine ndani ya kilabu walilala chini lakini Onchuru akasalia amesimama akijaribu kujitambua yeye ni afisa wa polisi.

Polisi hao walijitetea kuwa kulikuwa na makabiliano makali ndipo watatu hao wakapigwa risasi na kuuawa.

Jaji Mutuku, alisema ushahidi uliotolewa uliwalenga wawili hao.

“Washtakiwa hawajapinga kuwa ni wao walisababisha vifo vya Onchuru, Nyabuto na Okenye,” alisema Jaji Mutuku.

Mamlaka huru ya Polisi (IPOA) lilichunguza mauaji hayo na kumpendekezea  Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) awashtaki wawili hao kwa mauaji.

Wakiomba korti iwaachilie , washtakiwa hao walisema kuwa walikuwa wanashika doria walipoitwa kufahamishwa kulikuwa na wezi hatari katika kilabu hicho waliokuwa wamejihami kwa silaha.

Lakini Jaji Mutuku alisema marehemu walikuwa wamejisalamisha walipomiminiwa risasi na kutolewa uhai.

Jaji alisema hakukuwa na ufyatulianaji wa risasi.

Alisema washtakiwa walitumia nguvu kupita kiasi na kuwapata na hatia ya kuua wakikusudia.

You can share this post!

Greenpeace Africa: Miaka 10 ya kutunza mazingira

Kassachom motoni

adminleo