• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Safaricom yawafaa wanawake wajawazito

Safaricom yawafaa wanawake wajawazito

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kaunti ya Lamu imeingia kwenye mkataba wa maelewano (MoU) kati yake na wakfu wa Safaricom ili kujenga nyumba maalum zitakazotumika na akina mama wajawazito wakati wakisubiri kujifungua kwenye zahanati ya Witu.

Mradi huo wa gharama ya Sh 6.8 milioni unatarajiwa kuongeza idadi ya akina mama wajawazito wanaotafuta huduma za hospitalini, hivyo kupunguza vifo ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa  vya akina mama na watoto wakati wakijifungua.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi mjini Witu jana, Afisa wa wakfu wa Safaricom, Bi Janice Mwendameru, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika kufikia mwaka 2019.

Bi Mwendameru alisema vibanda hivyo vitatoa mwanya wa akina mama wajawazito kubaki karibu na hospitali angalau kwa siku kumi wakisubiri siku ya kujifungua.

“Kinyume na ilivyo sasa ambapo akina mama wajawazito huanza kuhangaika kwa usafiri kuja hospitali kujifungua hasa siku zao zinapowadia, vibanda tunavyonuia kuvijenga vitawawezesha akina mama hao kuja hospitalini mapema na kubaki kwenye vibanda hivyo hadi pale siku yao itakapofika. Tunaamini mradi huo utasaidia kuongeza idadi ya wanaojifungulia hospitalini na kupunguza vifo vya akina mama na watoto,” akasema Bi Mwendameru.

Akizungumza wakati wa halfa hiyo, Gavana wa Lamu, FahimTwaha alisifu wakfu wa Safaricom kwa juhudi zake katika kuboresha afya ya akina mama wajawazito na watoto.

Aliahidi ushirikiano wa dhati kati ya kaunti na wakfu wa Safaricom katika kuhakikisha maendeleo yanaafikiwa kote Lamu.

Bw Twaha alisema ili kupiga  jeki utoaji wa huduma za afya na kuwapunguzia wananchi ya matibabu, serikali yake  tayari imefadhili takriban familia 20,000 kwa bima ya kitaifa ya afya (NHIF).

“Nafurahia wakfu wa Safaricom kwa kuzingatia Lamu katrika ufadhili wake wa masuala ya afya. Tutashirikiana kwa dhati katika kuinua sekta hiyo eneo hili,” akasema Bw Twaha.

Mnamo Juni mwaka huu, wakfu wa Safaricom ulizindua mradi wa Sh 300 milioni wa kukabili vifo vya akina mama wajawazito na watoto kwenye kaunti tatu za kaskazini mwa Kenya, ikiwemo Lamu.

You can share this post!

Maziwa ya mursik hasababisha gonjwa la kansa – Utafiti

Nahodha wa Simbas kukosa mechi kali dhidi ya Hong Kong

adminleo