• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Hatimaye Mutua akubali kushirikiana na Ngilu na Prof Kibwana

Hatimaye Mutua akubali kushirikiana na Ngilu na Prof Kibwana

CHARLES WASONGA na STEPHEN MUTHINI

GAVANA wa Machakos, Dkt Alfred Mutua Ijumaa alikutana na wenzake, Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu wa Kitui katika kile kilichoonekana kama hatua ya kurejesha ushirikiano wake na viongozi wa Ukambani.

Mkutano huo uliofanyika mjini Machakos pia ulihudhuriwa na wanachama wa baraza la wazee wa jamii ya Wakamba, Maspika na viongozi wa mabunge ya Kaunti za Machakos, Kitui na Makueni.

Mwenyeji wa mkutano huo ambao pia ulijadili masuala ya maendeleo ya eneo hilo chini ya mwavuli wa Muungano wa Kiuchumi wa Ukanda wa Kusini Mashariki (SECEB), Askofu Mkuu wa Kanisa la ABC, alikuwa Timothy Ndambuki.

Askofu Ndambuki ni mwandani wa karibu wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye amekuwa akiendeleza mchakato wa kuwaleta viongozi wa Ukambani pamoja kuimarisha azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Gavana Mutua pia ametangaza kuwa atawania urais mwaka wa 2022 kwa tiketi ya chama chake cha Maendeleo Chap Chap (MCC), hatua ambayo wandani wa Bw Musyoka wanasema itaathiri mshikamamo wa kisiasa katika eneo la Ukambani.

Hata hivyo, katika ujumbe wake kwenye Facebook, Gavana Mutua alisema alikuwa na wenzake wawili kujadili masuala ya maendeleo katika kaunti hizo tatu.

“Leo (jana) nimekutana na majirani zangu na wenzangu Magavana Kivutha Kibwana wa Makueni na Charity Ngilu wa Kituo kujadili Muungano wa Kiuchumi wa Ukanda wa Kusini Mashariki (SECEB) na maendeleo ya ukanda huu kwa ujumla. Mkutano huu ulilenga kufufua muungano huo ambao pia utajumuisha viongozi kama vile maseneta, wabunge na madiwani,” akasema Dk Mutua.

“Naunga mkono kuimarishwa kwa muungano huo wa kimaendeleo kwa sababu utasaidia kaunti hizi tatu kuoanisha ajenda za maendeleo katika kusaidia kuondoa umasikini. Pia tutavutia ufadhili na usaidizi kutoka washirika wa maendeleo,” akaongeza.

Lakini wadadisi wa siasa za Ukambani sasa wanatizama mkutano huo kama jukwaa mwafaka la kuziba nyufa za kisiasa katika eneo la Ukambani lengo likiwa ni kuimarisha nafasi ya Bw Musyoka ya kuingia Ikulu.

“Maendeleo hayawezi kunawiri katika mazingira ya migawanyiko na uhasama wa kisiasa. Kwa hivyo, hatua ya Gavana Mutua kuamua kufanya kazi na viongozi wa kisiasa katika eneo la Ukambani itatusaini kutua jiwe moja kuwaua ndege wawili, umoja wa jamii yetu kisiasa na kuimarishwa kwa maendeleo,” akasema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Dkt Joshua Kivuva.

You can share this post!

Mzee afurushwa basini kwa kutazama video za ngono

Waluhya kamwe hawawezi kuungana, asema Khalwale

adminleo