• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
JAMVI: Kalonzo atakiwa aombe radhi waasi

JAMVI: Kalonzo atakiwa aombe radhi waasi

PIUS MAUNDU na KITAVI MUTUA

MZOZO uliogubika chama cha Wiper baada ya kinara Kalonzo Musyoka kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta unaendelea kutokota huku mwenyekiti wa chama Kivutha Kibwana sasa akimtaka Bw Musyoka awaombe msamaha waasi wa Wiper waliohamia Jubilee.

Prof Kibwana alisema haikuwa haki kwa Wiper kuwashawishi wafuasi wake kutupa wawaniaji wa Jubilee eneo la Ukambani kisha kinara wake ajiunge na ‘adui’ waliopinga.

Sasa Gavana huyo wa Makueni anamtaka Bw Musyoka kuwaomba msamaha wanasiasa wa Jubilee Ukambani kwa kuwabandika ‘waovu’ kisha awarudishe nyumbani.

Ushirikiano huo ulifichuka wiki jana wakati wa mazishi ya babake Bw Musyoka, Mzee Peter Mairu, nyumbani kwao Tseikuru mjini Mwingi, Kaunti ya Kitui.

Tangu siku hiyo Prof Kibwana ametofautiana na baadhi ya wanachama wa Wiper na kushutumu wazi wazi ushirikiano huo.

Prof Kibwana anataka chama hicho ambacho ngome yake ni eneo la Ukambani, kuwavutia wanasiasa waliowania uchaguzi kwa tiketi ya Jubilee.

Alifichua kwamba alikuwa miongoni mwa washauri ambao walikuwa wakimshinikiza Bw Musyoka kusaka mwafaka wa ushirikiano na serikali baada ya muungano wa upinzani NASA kushindwa na Jubilee katika uchaguzi mkuu mwaka jana.

Muungano huo ulijumuisha vyama tanzu vya Orange Democratic Movement (ODM), Wiper Democratic Movement (Wiper), Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya.

“Alijikokota na kwa sababu kinara wa ODM Raila Odinga ni mwerevu alinyaka fursa hiyo na kuingia katika mwafaka wa maelewano na Rais Kenyatta,” alisema Prof Kibwana katika ukumbi wa KICC mjini Nairobi.

Alikuwa akizungumza Ijumaa katika kikao cha wajumbe wa kutoka Makueni wanaoishi mjini Nairobi pamoja na viongozi wa Baraza la Wazee wa Akamba.

Bw Musyoka alitangaza kwamba yuko tayari kuwa kibaraka cha Bw Kenyatta baada ya Rais kudokeza kuwa atamteua kama balozi wa amani, wakati wa mazishi hayo.

Tangazo hilo liliibua mjadala mkali kutoka kwa wandani na wakosoaji wa Bw Musyoka na vile vile katika eneo la Ukambani ambako ni ngome ya Wiper.

Prof Kibwana amesisitiza kwamba ushirikiano mpya baina ya Rais Kenyatta na Bw Musyoka utaingilia azma ya makamu huyo wa zamani wa rais kuwania uongozi wan chi 2022.

Anataka mwafaka huo kutayarishwa upya ili kuleta manufaa ya hakika kwa jamii ya Wakamba, ikiwemo uteuzi katika nyadhifa za juu na miradi mikubwa ya maendeleo.

“Tunafaa kujiuliza nini kilichojadiliwa katika mwafaka huo? Nini tunataka kutoka kwa serikali?” akauliza Prof Kibwana ambaye pia ni Gavana wa Makueni.

Aliongeza: “Ni vyema kuwa na mazungumzo yanayofanywa kwa utaratibu. Ni vyema pia kusikia hoja za kila upande ili tupate kitu kinachofaa kutoka kwa serikali.”

Kikao hicho cha KICC pia kilijadili kiwango cha maendeleo katika kaunti hiyo na jinsi ya kuvuna kutokana na mwafaka mpya wa Rais Kenyatta na Bw Musyoka.

Kiliandaliwa na kundi la Makueni County Development Forum na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali ikiwemo Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, mbunge wa Makueni Daniel Maanzo na madiwani kadhaa.

You can share this post!

UAVYAJI MIMBA: Marie Stopes yazimwa

Itikadi zazuia wengi kuchukua bima ya mazishi wakiwa hai

adminleo