• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
TAHARIRI: Hapana! Tusikubali wabunge kutufilisi

TAHARIRI: Hapana! Tusikubali wabunge kutufilisi

Na MHARIRI

MPANGO mpya wa wabunge kutaka kujiongeza marupurupu na kudai maisha ya kifahari, unaonyesha jinsi ambavyo watu hao 416 waliochaguliwa na wananchi agosti 8, kamwe hawajali maslahi ya Mkenya.

Imebainika kuwa Tume ya Huduma za Bunge imeunda sheria inayopendekeza wabunge wapewe nyumba rasmi na serikali, la sivyo wapate narupurupu ya makao.

Mbali na hayo, wanataka magari yanayolipiwa kila kitu na mwananchi, japokuwa huwa wanapewa mikopo ya hadi Sh7 milioni kununua magari ya kifahari.

Malipo ya makao yatakuwa kando na mkopo wa Sh20 milioni wa nyumba ambao kila mbunge hupewa na kukatwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka. Wabunge pia wanalalamika kwamba hawapati manufaa ikilinganishwa na mawaziri na majaji.

Pia wanapendekeza waongezewe malipo ya bima ya matibabu ambayo itatoa huduma pia kwa jamaa zao wa mbali na wapenzi wa kando, mbali na marupurupu zaidi ya usafiri nchini na ng’ambo.

Mahitaji haya mengi wanayataka wabunge wakati ambapo kumekuwa hakuna mijadala ya maana bungeni. Tangu Machi mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wasalimiane kwa mkono, wabunge wote wamekuwa wakitekeleza yale yanayotakiwa na wawili hao.

Lengo la uwakilishi bungeni, mbali na kutunga sheria, ni kujadili masuala muhimu ya kitaifa kwa njia ya ukomavu, na kutafuta suluhu kwa matatizo yanayowakumba wananchi.

Kwa mfano sasa hivi, miongoni mwa masuala yanayomkabili Mkenya ni kupanda kwa gharama ya maisha. Ni juzi tu ambapo Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) iliongeza bei ya mafuta na kufikia Sh118 Nairobi, huku Wakenya walio miji ya mbali wakilipa hata Sh140 kwa lita.

Wabunge wanapaswa kujiuliza, kama walikataa asilimia 16 na ikapunguzwa hadi asilimia 8, ni kwa nini bei ya mafuta imerudi pale pale ilipokuwa wakati wa asilimia hiyo 16? Kwa nini wasiunde sheria itakayozuia ERC kupandisha bei ya mafuta kufikia kiwango fulani? Kawaida bei ya mafuta inapopanda, kila kitu bei yake hupanda moja kwa moja,

Viongozi hao wangekuwa wanatekeleza wajibu wao ipaswavyo, hakungekuwa na hata mwananchi wa kutaka kujua kwa nini wanajiongeza mshahara. Kwa sasa, huo ni ulafi ambao iwapo utariuhusiwa, tutakuwa tunaendelea hulka ya walio na uwezo kuendelea kuwakandamiza wasiokuwa na sauti.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Nitazima genge linalohangaisha wakazi...

OBARA: Ujeuri wa MCAs ni tishio kwa ufanisi wa ugatuzi

adminleo