• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
OBARA: Ujeuri wa MCAs ni tishio kwa ufanisi wa ugatuzi

OBARA: Ujeuri wa MCAs ni tishio kwa ufanisi wa ugatuzi

Na VALENTINE OBARA

HUKU wananchi wengi wakishikilia imani kwamba ufisadi ndio tishio kubwa zaidi kwa mafanikio ya ugatuzi, kuna tishio jingine ambalo lisipokabiliwa litatusababishia majuto katika siku za usoni.

Wakati Katiba iliporekebishwa na hatimaye kupitishwa katika mwaka wa 2010, mabunge ya kaunti yalikabidhiwa mamlaka makubwa mno ya kusimamia shughuli za afizi za magavana katika kaunti zetu 47.

Kipindi cha kwanza cha utawala wa ugatuzi kilichoanza 2013 kilishuhudiwa matukio ya kuchukiza katika mabunge hayo, kwani ilidhihirika wazi kuwa madiwani wengi waliochaguliwa walikuja na zile tabia mbovu walizokuwa nazo wakati walipokuwa viongozi katika mabaraza ya miji.

Mwaka uliopita, ilitarajiwa wananchi wangekuwa wamejanjaruka vya kutosha kuchagua madiwani wenye maadili mema na mienendo ya kistaarabu inayofaa kwa uongozi bora, lakini hali sivyo.

Madiwani wamepewa majukumu muhimu ambayo yanaweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi mashinani kwa kuhakikisha kuna sera mwafaka na usimamizi bora wa rasilimali za umma katika kaunti zetu.

Kinachosikitisha ni kuwa viongozi hawa wametambua ukuu wa majukumu yao lakini badala ya kuutumia ipasavyo, wameamua kuyatumia kwa masilahi yao ya kibinafsi.

Kwa miezi kadhaa sasa, kumekuwa na mizozo katika mabunge ya kaunti nyingi zikiwa ni pamoja na Nairobi, Nyandarua, Homa Bay, Machakos na Kisumu ambako kulitokea hata ufyatuaji wa risasi.

Tathmini ya kina kuhusu mizozo hii inaonyesha kuwa haisababishwi na juhudi za kutetea haki za wapigakura bali ni mbinu za madiwani kushinikiza matakwa ya kujaza matumbo na mifuko yao.

Unapodadisi kwa kina, utatambua malalamishi yao mengi ni kuhusu marupurupu, mikopo ya nyumba na magari, au hata kutengewa fedha za kusafiri kuenda ng’ambo kwa ziara ambazo hazina umuhimu wowote kwa umma.

 

Kunga’atua maspika

Tofauti na jinsi ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza cha utawala wa ugatuzi ambapo vitisho vya madiwani vilielekezwa kwa magavana kupitia kwa majaribio ya kuwang’oa mamlakani, wakati huu wamebadili mbinu na kuelekeza jeuri yao kwa maspika wa mabunge ya kaunti.

Hatua hii huenda imetokana na jinsi wametambua si rahisi kuondoa gavana mamlakani kisheria kupitia kwa mswada wa kutokuwa na imani kwa utawala wake, ndiposa wanalenga maspika ambao hawana ulinzi mkubwa mamlakani ikilinganishwa na magavana.

Ningefurahi sana iwapo ningeona madiwani wakizozana kwa msingi wa ufichuzi wa sakata za ufisadi katika kaunti au kwamba gavana ametumia mamlaka yake kwa njia inayoathiri vibaya maendeleo ya kaunti.

Mambo haya ni nadra kuona yakijitokeza katika mabunge ya kaunti na hivyo basi hatuna budi kuchukulia kwamba wao ni washirika wa maovu yanayoendelezwa katika baadhi ya afisi za magavana ambayo hufichuliwa na asasi za serikali kuu au vyombo vya habari.

Iwapo mambo yataendelea jinsi hii, basi itakuwa ni heri madiwani wapunguziwe mamlaka ili kufanikisha ugatuzi.

Madiwani wamejionyesha kuwa viongozi wasioweza kudhibitiwa kivyovyote, na kupunguziwa mamlaka ndiko kutaokoa umma.

You can share this post!

TAHARIRI: Hapana! Tusikubali wabunge kutufilisi

KURUNZI YA PWANI: Waganga 20 sasa waililia serikali...

adminleo