• Nairobi
  • Last Updated April 22nd, 2024 8:55 PM
#MheshimiwaFisi: Wabunge wapapurwa mitandaoni kujaribu kujiongezea mishahara

#MheshimiwaFisi: Wabunge wapapurwa mitandaoni kujaribu kujiongezea mishahara

Na PETER MBURU

WAKENYA kwenye mitandao ya kijamii wameanzisha vita dhidi ya wabunge ambao wanaunga mkono mjadala wa kujiongezea mshahara bungeni, wakitumia picha na maneno yaliyowarejelea viongozi hao kuwa fisi.

Kupitia kwa hashtegi #MheshimiwaFisi katika mtandao wa Twitter, mamia ya Wakenya waliwakashifu viongozi hao kwa kuwa na ubinafsi na kutojali maslahi ya wananchi masikini ambao wanateseka, badala yake wakijali tu kujiongezea pato lao.

Wabunge wanapendekeza kupata huduma kadha ghali kwa gharama ya mlipa ushuru, licha ya hali kubwa ya umasikini ambayo Wakenya wengi wako katika.

Kampeni hiyo ilishika kasi huku picha za wabunge mbali mbali zikigeuzwa sehemu ya mdomo usoni na kupachikwa mdomo wa fisi uliopanuliwa, kuashiria ulafi walio nao wabunge.

Picha hizo za viongozi mbalimbali ziliandamana na maneno aina aina, yote kuwakashifu wabunge waliotetea kuongezewa mapato.

“Mwananchi anaelekea kufa chini ya mzigo wa mishahara uliopo sasa lakini bado mnataka kujiongezea mishahara #MheshimiwaFisi,” akasema Polycarp Hinga @PolycarpHinga.

“Wabunge hawa pia wanataka kupewa bima ya matibabu kukinga hata zaidi ya mke mmoja na watoto wanaozaliwa nje ya ndoa #MheshimiwaFisi,” HAVANA @havana-gg akasema.

Baadhi ya wananchi walitofautiana na kauli kuwa viongozi ni picha ya jamii wanayowakilisha, wakisema wa Kenya wamekuwa wabinafsi.

“Hata kama inasemekana viongozi huakisi jamii, wanasiasa wetu ni kitu kingine. Mtu anaweza kudhani wao ni watoto wa nguruwe na fisi #MheshimiwaFisi,” akasema Mwangi X Muthiora @MwangiMuthiora.

Baadhi ya watu walieleza kuwa viongozi wamesaliti wapiga kura kwa kugeuka baada ya kuchaguliwa.

“Tulidhani lengo lenu lilikuwa kutuwakilisha lakini inavyooonekana mnataka kutula,” Bella @Anabell58649080 akasema.

Wabunge walioaibishwa katika kampeni hiyo ni wa Moiben, Joash Nyamoko wa Mugirango Kaskazini, Gladys Wanga (Homa Bay), Sabina Chege (Murang’a), Millie Odhiambo (Mbita), Moses Kuria (Gatundu Kusini), John Waluke, Peter Kaluma, Catherine Waruguru kutoka Laikipia miongoni mwa wengine.

“Ikifika ni kutupora wanaungana kabisa lakini ikifika ni kujihusisha na masuala kuhusu maslahi yetu kila mtu ni kujitetea na tunaachiwa Mungu, hawa ni ‘Waheshimiwa fisi’.”

Kibet Benard @KibetBenard naye alisema “#MheshimiwaFisi analilia mshahara zaidi wakati Wakenya wanapambana na maisha.”

You can share this post!

DPP aishangaa mahakama kumwachilia huru Obado

HONGO BUNGENI: DCI na EACC kuchunguza wabunge wanaodaiwa...

adminleo