• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:40 AM
Nirudisheni Juventus, Pogba aiambia Man United

Nirudisheni Juventus, Pogba aiambia Man United

LONDON, Uingereza

NYOTA Paul Pogba, 25, amewataka Manchester United kumwachilia mwishoni mwa msimu huu ili arejee jijini Turin, Italia kuwapigia soka miamba wa Ligi Kuu ya Serie A, Juventus.

Juventus wapo radhi kumsajili upya kiungo huyu mzawa wa Ufaransa na tayari wamewasilisha ombi la kuanzisha mazungumzo rasmi na usimamizi wa Man-United.

Pogba aliwahi kuagana na Man-United na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Juventus kwa misimu minne kabla ya kurejea jijini Turin Oktoba akiongoza kikosi cha kocha Jose Mourinho kuchapana na magwiji hao wa Serie A katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League).

Man-United walisajili ushindi wa 2-1 katika pambano hilo lililomshuhudia nyota wa zamani wa Man-United, Cristiano Ronaldo akitikisa nyavu za waajiri wake hao wa zamani.

Japo wakala Mino Raiola amemtaka sana mteja wake kuhamia Barcelona nchini Uhispania, Pogba amepania kurejea Juventus hasa ikizingatiwa kauli yake ya hivi majuzi akikiri kuyafurahia maisha yake nchini Italia.

Kiini cha Pogba kutaka sana kubanduka uwanjani Old Trafford ni kufarakana kwake na Mourinho ambaye amekosolewa sana na baadhi ya wachezaji nyota wa Man-United kutokana na mbinu zake za ukufunzi.

Kwa upande wake, kocha Massimiliano Allgeri wa Juventus ameungama kuwa kukosekana kwa Pogba kambini mwa kikosi chake kulichangia sana kushindikana kwa juhudi zao za kutwaa ubingwa wa UEFA msimu jana.

Ili kuweka hai matumaini ya kutia kapuni ubingwa wa taji hilo muhula huu, Juventus walimvua Ronaldo kutoka Real Madrid, jambo ambalo kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia na Uingereza, huenda yakamnyima Pogba fursa ya kurejea Italia kuvalia jezi za Juve kwa mara nyingine kwa sababu za uwezo wa Juve kumudu kugharimia mishahara yao kwa pamoja. Ronaldo ni mmoja wa wasakataji wanaopata mshahara wa juu zaidi duniani kwa sasa.

Kulingana na gazeti la Corriere dello Sport nchini Italia, Pogba ameanza tayari kuwasiliana na baadhi ya wachezaji wa Juventus akiwahakikishia uwezekano wa kurejea kwake kambini mwa kikosi hicho.

Sogora huyu amekuwa nje ya kampeni za Ufaransa katika kivumbi cha Nations League wiki hii na huenda akaunga kikosi cha kwanza cha Man-United dhidi ya Crystal Palace wikendi hii.

Mbali na Pogba, Alexis Sanchez na Anthony Martial, Man-United huenda pia wakaagana na kipa David De Gea ambaye dalili zote zinaashiria kwamba ana kiu ya kubanduka Old Trafford.

Man-United wamepania kujinasia huduma za Mwingireza Jordan Pickford wa Everton kujaza pengo la De Gea ambaye amekataa kutia saini mkataba mpya ambao amekuwa akishawishiwa kwa miezi kadhaa kutia saini ugani Old Trafford.

Kiini cha De Gea kutaka kuagana na ?kikosi hicho cha Mourinho ni kusitasita kwa usimamizi kumpa uhakika wa nyongeza ya mshahara utakaokaribiana na ule wa Sanchez ambaye kwa sasa anapokea ujira wa takriban Sh42 milioni kwa wiki bila marupurupu wala bonasi.

Man-United wanahisi kwamba Pickford ndiye chaguo bora zaidi katika juhudi za kulijaza pengo la De Gea anayewaniwa pakubwa na Juventus.

You can share this post!

Wandani wa Ruto wasema wanaompinga wamelipwa na Moi

Wabunge watishia kumuadhibu Matiang’i

adminleo