• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
ZAC ABDALLAH: Kipaji cha kipekee cha uchoraji

ZAC ABDALLAH: Kipaji cha kipekee cha uchoraji

Na PAULINE ONGAJI

Kilichoanza kama jambo la kupitisha muda utotoni, sasa kimegeuka na kuwa kipaji na taaluma ambayo inampa riziki ya kila siku.

Kutana na Zac Abdallah, 25, mchoraji mjini Mombasa anayechora kwa kutumia penseli pekee na kuleta uhalisi wa nyuso za watu kwenye turubai.

Ni kazi ambayo imemletea umaarufu katika eneo la Old Town, jijini Mombasa anakoendeleza shughuli zake.

Kinachoshangaza hata zaidi ni kuwa kipaji hiki ni cha kujifunza na kamwe hajasomea uchoraji huku ustadi wake ukidhihirika kupitia picha za watu maarufu aliowachora.

“Baadhi ya watu ambao nimechora ni pamoja na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, mfanyabiashara Aharub Khatri na mpishi Ali Mandhri,” aeleza.

Lakini ustadi wake haujahusisha watu maarufu pekee kwani pia anachora picha anazoagizwa na wateja wa kawaida huku akipata riziki kidogo kutokana na kazi hii.

“Kwa kawaida mimi hulipisha Sh 5000 kwa picha ya ukubwa wa sentimeta 50 kwa 50 huku ikimchukua takriban siku tatu kukamilisha kazi moja ya aina hii,” aeleza.

Lakini kutokana na sababu kuwa ni miezi sita tu tangu alipojitosa katika sanaa kama mtaalam bado hajapata wateja wa kutosha kumaanisha kwamba kipato bado sio thabiti.

Kazi ya Zac Abdalla. Picha/ Pauline Ongaji

Hii ni mojawapo ya changamoto ambazo zimekuwa zikimkumba mchoraji huyu kwani
licha ya kushamiri na kuonyesha ujuzi wa hali ya juu, kazi hii haijamwezesha kujisimamia vyema kifedha.

Ni suala ambalo huenda likakatiza ndoto yake ya kuendelea katika tasnia hii hasa ikizingatiwa kuwa anasema iwapo mambo hayatabadilika huenda akalazimika kujitosa katika taaluma ya uhasibu ili kujitafutia mapato zaidi.

“Sisemi kwamba napanga kugura taaluma ya uchoraji kabisa lakini huenda ikawa kazi yangu ya kando endapo nitajitosa katika uhasibu,” aeleza.

Ni tatizo hili ambalo limetatiza shughuli zake za kuwa na chumba cha kuhifadhi sanaa zake vile kutokuwa na uwezo wa kuandaa maonyesho ya kazi zake.

Mbali na hayo analalama kwamba sio rahisi kuwa mwanasanaa hasa   mjini Mombasa hasa ikizingatiwa kuwa sio watu wengi wanaoelewa umuhimu wake.

“Kutokana na hili ni ngumu sana kupata wateja walio tayari kutumia pesa nyingi kununua kazi zangu, suala ambalo bila shaka limeathiri mapato sio yangu tu bali ya wanasanaa wengine,” aeleza.

Abdallah alianza kuchora tangu utotoni ambapo anakumbuka akijihusisha na uchoraji kwa mara ya kwanza akiwa na miaka minane pekee.

Kulingana naye mwanzoni alianza kuifanya ili kupitisha muda huku uchu wake ukichangiwa na kiu chake cha kutaka kufanikiwa katika tasnia hii.

“Kuna wachoraji wengi waliochochea ari yangu lakini kigezo changu kikuu kilikuwa mwanasanaa Tony Mahfud kutoka Ujerumani,” aeleza.

Mbali na uchoraji ni mtaalam wa masuala ya usanifu kurasa. “Katika ulingo huu kazi yangu inahusisha kusanifu vocha, kadi za kibiashara, nembo na brosha ambapo nimetoa huduma zangu kwa kampuni kadha na watu binafsi,” aeleza.

Kadhalika amepiga nakshi taaluma yake ya sanaa ambapo sasa pia anajihusisha na uchoraji katuni huku kazi zake zikihusishwa kwenye vitabu kadha vya watoto.

“Kwa sasa niko katika harakati za kufanyia kazi kitabu changu cha kwanza kwa jina Adventures Of Sam and Pig. Hii ni kando na ndoto yangu ya pia kuwa mwanamitindo, aeleza.

Lakini zaidi ya yote anasema kwamba uchoraji unasalia kwa kipaji chake murwa na anafanya kila awezalo kuhakikisha kwamba licha ya matatizo yanayomkumba anahifadhi kipaji hiki.

“Katika kipindi cha miaka michache ijayo najiona nikishamiri kama mchoraji maarufu hasa nikiendesha shughuli zangu jijini Dubai,” aeleza.

You can share this post!

Aspirin inaweza kupunguza maambukizi ya HIV – Utafiti

IEBC imeoza, hapa uvundo tu – Chiloba

adminleo