• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
IEBC imeoza, hapa uvundo tu – Chiloba

IEBC imeoza, hapa uvundo tu – Chiloba

Na WYCLIFFE MUIA

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Ezra Chiloba Alhamisi alifichua uozo zaidi uliokumba tume hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, akisema makamishna wote wa IEBC walikosa maadili katika utendakazi wao.

Akijitetea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC), Bw Chiloba alidai kuwa baadhi ya makamishna akiwemo mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, waliingilia na kushawishi utoaji wa zabuni wakati wa uchaguzi ili kujifaidi binafsi.

“Nimefanya kazi na makamishna wote wa IEBC na bila kusita nitasema kuwa hawana maadili ya uongozi, haswa mwenyekiti mwenyewe,” alisema Bw Chiloba.

Alidai kuwa Bw Chebukati alitumia wadhifa wake kupatia kampuni yake ya mawakili kandarasi sita za kuwakilisha IEBC katika kesi kuhusu uchaguzi wa 2017.

“Mwenyekiti alidai kuwa alijiuzulu katika kampuni yake ya mawakili lakini alikosa maadili kwa kuipatia kandarasi bila kuelezea uhusiano wake na kampuni hiyo wakati wa utoaji zabuni hiyo,” alisema Bw Chiloba

Bw Chiloba pia alidai Bw Chebukati alijaribu kumshawishi atoe kandarasi ya kuchapisha karatasi za kura kwa kampuni ya Reflon yenye makao makuu Afrika Kusini.

“Makamishna wote waliketi na kuniagiza nitafute kampuni ya kuchapisha kandarasi za kura. Baadaye mwenyekiti aliniita afisini mwake na kunipa stakabadhi za kampuni ya Reflon, ambayo alinitaka niipatie kandarasi hiyo. Siku mbili baadaye alinitumia barua pepe akitaka kujua nimefikia wapi katika utoaji kandarasi hiyo” alidai Bw Chiloba.

Alisema alikataa kuipatia kampuni hiyo kandarasi kwa sababu huo haukuwa msimamo wa makamishna wote wa IEBC, na hapo ndipo masaibu yake na mwenyekiti huyo yalipoanza.

“Siku mbili baadaye, mahakama iliidhinisha kampuni ya Al Ghurair kuchapisha karatasi hizo na mara moja tukaipatia kazi,” alieleza Bw Chiloba.

Bw Chiloba, ambaye alisimamishwa kazi Oktoba mwaka huu, alidai kuwa makamishna wa tume hiyo walikuwa wanakutana na baadhi ya wafanyabiashara kisiri ili kushawishi utoaji zabuni katika IEBC.

Alipoulizwa iwapo mwenyekiti pamoja na makamishna watatu waliobaki katika IEBC wanafaa kuendelea na kazi, Bw Chiloba alisema watatu hao ndio ‘kiini’ cha uovu katika IEBC.

“Sera na sheria hazina maana iwapo wanaoongoza hawana maadili ya uongozi. Maoni yangu ni kuwa kuna shida kubwa ya uongozi katika IEBC,” aliongeza Bw Chiloba.

Madai ya Bw Chiloba  yalikinzana na kauli za Bw Chebukati, ambaye alipofika mbele ya PAC siku ya Jumatatu alidai kuwa makamishna wa tume hiyo hawakushauriwa kuhusu zabuni zilizotolewa na Bw Chiloba.

Bw Chebukati alisema Bw Chiloba na maafisa wake walikiuka sheria za kutoa kandarasi hali iliyopelekea tume hiyo kupoteza mabilioni ya pesa.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa serikali Edward Ouko ilisema kuwa zaidi ya Sh9 bilioni hazijulikani zilivyotumiwa na IEBC wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.

Jana, mwenyekiti wa PAC, Opiyo Wandayi alisema kamati hiyo imemtaka aliyekuwa mkuu wa masuala ya kisheria katika IEBC, Praxedes Tororey kufika mbele yake wiki ijayo.

Bw Wandayi alisema baadaye kamati hiyo itaandaa ripoti yake kuhusu ‘uozo’ katika IEBC na kuifikisha bungeni ili kujadiliwa.

Makamishna watatu Connie Nkatha (Naibu Mwenyekiti), Ms Margaret Mwachanya na Paul Kurgat tayari wamejiuzulu kutoka kwa tume hiyo.

You can share this post!

ZAC ABDALLAH: Kipaji cha kipekee cha uchoraji

Matatu zafungiwa nje ya katikati ya jiji, wakazi kuhangaika...

adminleo