• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
Wabunge na maseneta kumumunya Sh400 milioni michezoni Burundi

Wabunge na maseneta kumumunya Sh400 milioni michezoni Burundi

CHARLES WASONGA na PETER MBURU

HUKU nchi inapoendelea kuzongwa na changamoto za kifedha, wabunge na maseneta wamesafiri nchini Burundi kwa michezo baina ya mabunge ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanzia Jumamosi, ambapo watatumia takribani Sh400 milioni pesa za mlipa ushuru.

Timu ya Kenya inayojumuisha wabunge, maseneta na wafanyakazi wa bunge 390 imewasili jijini Bujumbura tayari kwa mashindano yatakayodumu siku kumi hadi Desemba 10.

Ijumaa, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alikejeli ziara hiyo ya viongozi ambayo itaacha taifa na gharama nyingine, licha ya kuwa haina faida ya moja kwa moja kwa uchumi wa taifa wala kuchangia kuinua viwango vya michezo nchini

Kwa lugha ya kejeli, Bw Kuria alirejelea kiwango kikubwa cha pesa kitakachotumika kwenye ziara hiyo na kushangaa manufaa yake.

“Kenya kweli ni taifa la michezo. Kuanzia wikendi hii kwa siku 10 zijazo, Kenya itatuma timu ndogo ya maseneta, wabunge na wafanyakazi wa bunge 390 kwa michezo ya mabunge chini Burundi. Sina shaka tutafanya vyema katika michezo hiyo haswa ule mchezo wa kuvuta kamba ambapo timu yetu ina washiriki wakubwa na wenye nguvu. Mje na mataji na mtumie vizuri Sh400milioni za kugharamia shughuli hizo vizuri. Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi sharti watutambue,” Bw Kuria akaandika kwenye akaunti yake ya Facebook jana.

Vilevile, alipozungumza na Taifa Leo, mbunge huyo alithibitisha madai yake kuwa ya kweli na kwamba, spika wa bunge Justin Muturi na wasimamizi wengine wa bunge wameidhinisha shughuli hiyo na gharama zote.

“Mimi nimepaza sauti na ambaye anaweza kudhani kuwa ni udaku wangu aulize spika wa bunge ama wasimamizi wengine wanaohusika na mambo hayo,” Bw Kuria akasema.

“Ni kweli kwamba wabunge wengi wamesafiri kwenda Burundi kwa michezo kati ya mabunge ya mataifa ya Afrika Mashariki, hali inayoomaanisha kuwa shughuli za mabunge yote mawili zitatatizika kuanzia Jumatatu. Hii ni kutokana na idadi ndogo ya waliosalia,” akathibitisha afisa mmoja wa bunge ambaye aliomba tulibane jina lake.

Bunge linatarajiwa kuahirisha vikao vyake Alhamisi Desemba 6, kwa likizo ndefu ya Chrismasi na Mwaka Mpya. Watarejea Februari 5 mwakani.

Sh400 milioni zinatarajiwa kugharamia nauli ya ndege, chakula, malazi, burudani na marupurupu ya wabunge hao pamoja na wahudumu wa bunge wanaoandamana nao.

Ziara ya Wabunge nchini Rwanda inajiri miezi miwili baada ya Spika Justin Muturi kufutilia mbali ombi la wabunge wanachama wa timu ya Voliboli la kutaka kusafiri hadi Tokyo, Japan kutizama mchuano wa Shirikisho la Voliboli Ulimwenguni (FIVB).

Bw Muturi alisema ziara hiyo haikuwa na maana kwa ustawi wa mchezo huo nchini. Ziara hiyo pia inajiri miezi mitano baada ya wabunge na maseneta 20 kwenda nchini Urusi kutazama michuano ya Kombe la Dunia kwa gharama ya Sh25 milioni, pesa za mlipa ushuru.

Lakini walisisitiza kuwa awalikwenda Urusi kujifunza jinsi Kenya inaweza kuandaa michuano ya hadhi na kiwango hicho.

Wananchi walikerwa na ziara ya wabunge hao baada Seneta Maalum Milicent Omanga na mwenzake James Orengo wakiwepa picha mitandaoni zikiwaonyesha wakijivinjari na mashabiki wa soka huko Urusi.

Waliporejea wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Michezo Victor Munyaka waliandaa ripoti bandia iliyodondolewa kutoka tovuti mbalimbali za michezo.

You can share this post!

MOSES DOLA: Mwanahabari ndani mwongo mzima kwa mauaji

Magufuli afuata nyayo za muafaka kuzima upinzani

adminleo