• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Magufuli afuata nyayo za muafaka kuzima upinzani

Magufuli afuata nyayo za muafaka kuzima upinzani

Na PETER MBURU

RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli anaonekana kufuata nyayo za mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta kuzima upinzani, baada ya hatua zake za majuzi kumvuta karibu kiongozi wa upinzani nchi hiyo Edward Lowassa.

Siku za hivi karibuni, Rais Magufuli na Bw Lowasa wameonyesha ushirikiano wa karibu sana, huku wote kila wanapozungumza wakionyesha hulka ya kusifiana, jambo linaloashiria kuwa hakuna tofauti baina yao.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakikutana mara kwa mara, na katika mkutano wao wa punde zaidi, Rais Magufuli alimsifu Bw Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wan chi hiyo mbeleni, kuwa kiongozi anayeendesha siasa za kwa njia ya ustaarabu, naye Bw Lowassa akimsifu Rais kuwa mchapakazi.

Hii ni licha ya wawili hao kuweka ushindani mkubwa katika uchaguzi wa taifa hilo mnamo 2015, ambapo kulishuhudiwa utengano baina ya upinzani na serikali.

Ndoa yao inaripotiwa kuanza Januari 9, mwaka huu wakati Bw Lowassa alialikwa katika ikulu ya taifa hilo na kufanya mazungumzo ya kina na Rais Magufuli lakini siku za hivi majuzi imeonekana kupata mnato zaidi.

Uhusiano wa wawili hao sasa unaonekana kushika nakshi hata zaidi baada ya kuona ule wa Rais Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu humu nchini Raila Odinga ukifanikiwa na kutuliza joto la siasa za nchi, japo Rais Magufuli amekuwa na tabia zilizoonekana kuwa za kidikteta na baadhi ya wadadisi.

Wadadisi wa siasa za nchi hiyo wamesema kuwa wawili hao wanachezea karata zao chini, japo hawaamini Rais Magufuli yuko tayari kabisa kuumeza upinzani kikamilifu.

“Rais Magufuli ni mwanasiasa mzuri kama ilivyo kwa Lowassa. Kikubwa ninachokiona hapa ni kwamba Rais Magufuli anajaribu kutuonyesha kwamba Lowassa ni mpinzani na yeye hana ugomvi na wapinzani. Lakini nyuma ya pazia tunaona wapinzani wanavyosumbuliwa, wengine wanakabiliwa na kesi nyingi mahakamani,” amesema mdadisi wa siasa Sammy Ruhuza kutoka Tanzania.

Tayari, Rais huyo ametoa onyo kwa viongozi wa upinzani kuwa kuzidisha pingamizi dhidi ya serikali ni kualika kukamatwa na kupelekwa gerezani.

Lakini upande wa upinzani umekuwa na imani kama zilizokuwa humu nchini miongoni mwa wafuasi wa NASA kuwa kiongozi wao ndiye alishinda uchaguzi. Wengi wa viongozi hao Tanzania wanaamini Bw Lowassa alishinda uchaguzi wa 2015.

Lakini licha ya wafuasi wake kuamini kuwa alishinda, hali yake ya kukosa kulalamika ama kumwekea Rais Magufuli visiki anapoongoza imewafanya baadhi ya wadadisi kuona kuwa ndiyo imemfanya Rais huyo kumvuta na kufanya kazi naye.

“Sasa unapomwona mwanasiasa huyu anaendelea kuwa mtulivu na wala hajaingia katika purukushani zozote lazima wewe uliyeshindana naye ujirudi na kujiuliza mara mbili na ndiyo maana tunaona Rais amekuwa akimwagia sifa mara kwa mara,” akasema Richard Mbunda, mhadhiri.

Wengi wa Watanzania walitarajia kuwa Bw Lowassa angeongoza maandamano ya pingamizi kwa serikali ya Rais Magufuli lakini hilo halikutendeka.

Badala yake, kiongozi huyo ndiye alikuwa wa kuwatuliza wasishiriki vitendo vya kuvunja sheria.

Majuzi, Rais Magufuli alisema kuwa serikali yake inahitaji viongozi wa upinzani waliokomaa kama Bw Lowassa kwa kuwa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2015 alikubali matokeo.

Hata hivyo, hakuwa na msamaha kwa waliokuwa nyuma yake ambao alisema “waliokuwa wakimpigia kampeni ndio waliokuwa na maneno” na kumtuma Bw Lowassa na ujumbe kwao kuwa wakiendelea “wataishia gerezani.”

Tayari, kuna baadhi ya viongozi ambao wamekamatwa na polisi siku za mbeleni kwa kupinga serikali, lakini Rais Magufuli sasa anaonekana kushughulika na kiongozi wao Bw Lowassa ambaye anamwona mkomavu na mwenye ushawishi mkubwa kitaifa.

Hatua ya Rais huyo ni sawa na aliyochukua Rais Kenyatta wakati joto la siasa nchini Kenya lilikuwa limepanda kupita kiasi, kwani tangu alipoafikiana na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018 kumekuwa na utulivu wa kisiasa, huku viongozi kutoka upande wa upinzani wakivuna.

Tangu kuafikiana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga, wa pili amepata kazi katika Muungano wa Afrika (AU), mwenzake Kalonzo Musyoka kufanywa balozi wa kutafuta amani Sudan Kusini n ahata viongozi wa upinzani kuanza kushirikiana na wale wa serikali katika baadhi ya maamuzi ambayo mbeleni walitengana vikubwa.

Inatarajiwa kuwa hata Tanzania Rais Magufuli atafuata mkondo huohuo anapolenga kuwavuta viongozi zaidi kutoka upande wa upinzani, huenda mwishowe upinzani ukimalizwa katika mataifa haya mawili.

You can share this post!

Wabunge na maseneta kumumunya Sh400 milioni michezoni...

Mtahiniwa wa KCSE atisha kuwaua Rais Kenyatta na Aden Duale

adminleo