• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Serikali yaondoa kondomu zenye mashimo madukani

Serikali yaondoa kondomu zenye mashimo madukani

Na CAROLYNE AGOSA

WIZARA ya Afya imetoa tahadhari dhidi ya matumizi ya kondomu za Fiesta baada ya mipira hiyo ya mapenzi kupatikana kuwa na mashimo.

Aidha, uchunguzi ulipata kuwa kondomu hizo zinazotumiwa na wanaume hazikuwa na unene unaohitajika.

Kasoro hizo katika kondomu za Fiesta Stamina na Fiesta Big Black ziligunduliwa wakati wa uchunguzi uliofanywa na Bodi ya Dawa na Sumu (PPB).

“Bodi ya Dawa na Sumu ilifanya uchunguzi uliojumuisha bidhaa za Fiesta Stamina na Fiesta Big Black zinazotengenezwa na kampuni ya Cupid Limited. Bidhaa za Fiesta Stamina zilikosa kutimiza kipimo cha kutokuwa na mashimo, huku Fiesta Big Black zikikosa kutimiza kipimo cha unene,” ilisema barua ya bodi hiyo iliyoandikwa Novemba 20, 2018 na kutiwa saini na afisa Jacinta Wasike kwa niaba ya Afisa Mkuu Mtendaji.

Iliongeza: “Unaagizwa kuondoa sokoni mara moja bidhaa zilizoathiriwa. Vile vile, unatakiwa kuwasilisha utaratibu wa jinsi utakavyoondoa bidhaa hizo katika siku mbili za kupokea barua hii.”

Kondomu za Fiesta zinatengenezwa na kampuni ya kimataifa ya Cupid Limited yenye makao yake nchini India, na kusambazwa katika mataifa zaidi ya 40 kote ulimwenguni. Kampuni hiyo pia huunda kondomu za wanawake.

Bidhaa za Fiesta ambazo ndizo huuzwa Kenya ni za aina na misisimko mbalimbali.

Zilizopatikana na kasoro za Stamina ni za rangi nyeusi, zenye madoadoa na kuleta msisimko wa “vanilla”.

Fiesta Big Black ni pana na ndefu zaidi kwa wanaume waliojaliwa mlingoti mkubwa chumbani.

Kwa mujibu wa maelezo katika tovuti yake, kondomu zote za wanaume ziko na kiungo kidogo cha Benzocaine ambacho humfanya kukawia kufika kileleni ili kula uhondo zaidi wa mapenzi.

Taarifa hizi zinakujia huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Ukimwi hii leo.

Kondomu zilizo na kasoro ni hatari kwani hukosa kuwapa wapenzi ulinzi wanaohitaji kuzuia mimba na vile vile maambukizi ya maradhi ya zinaa ikiwemo HIV.

Ripoti ya Ukimwi ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi (UNaids) 2017 inaashiria kuwa licha ya matumizi ya kondomu kuongezeka kila mwaka nchini, bado taifa halijatimiza shabaha yake ya asilimia 100.

Ni asilimia 73 ya wanaume na 55 ya wanawake pekee waliotumia kondomu mara ya mwisho waliposhiriki ngono na wapenzi ambao sio waume/wake zao rasmi.

Hatari zaidi ni kwamba, suala la “sponsa”, ambapo wanawake wachanga wanajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wanaume wazee ili kupata pesa, limechangia pakubwa katika kudidimiza kasi ya matumizi ya kondomu nchini.

Visa vya kondomu duni pia viliripotiwa mwezi Februari na shirika la Population Services Kenya (PSK).

Shirika hilo la afya ambalo husambaza kondomu za Trust nchini lilionya kuhusu kondomu zake feki zilizokuwa zikiuziwa wananchi.

You can share this post!

Mtahiniwa wa KCSE atisha kuwaua Rais Kenyatta na Aden Duale

Fisi waliolishwa sumu wavamia wakazi

adminleo