• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Mashabiki wa Ingwe wakaribisha kocha mpya kwa matusi na vitisho

Mashabiki wa Ingwe wakaribisha kocha mpya kwa matusi na vitisho

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wamemkaribisha kocha mpya wa AFC Leopards Marko Vasiljevic na mshambuliaji mpya Lawrence Luvanda shingo upande Jumamosi.

Huku mechi ya ufunguzi dhidi ya Kariobangi Sharks ikinukia hapo Jumapili mjini Machakos, mashabiki wameonyesha kutoridhika kwao na kuajiriwa kwa wawili hawa.

“Mpishi amefika…chakula cha jioni kitaandaliwa hivi karibuni,” alisema Mor Ris baada ya Leopards kutangaza kuwasili kwa raia wa Serbia, Vasiljevic. Kutokana na tabia ya Ingwe kufursha makocha kila uchao Pretty Doll aliuliza, “Atarejea lini kwake?”.

Naye Denno Dennice aliuliza kama Leopards ilikuwa ikifanya mzaha kwa kutangaza kuwasili kwa Vasiljevic, huku Jon Zelalem Okoth akimkumbusha kwamba, “Kuajiriwa na kufutwa ni rahisi sana Leopards.” Baadhi ya mashabiki walitarajia awe mtu mzee. Wanasema wamechangiwa kama Vasiljevic ni kocha ama mchezaji pengine kutokana na wembamba wake na sura ya mtu kijana.

Godfrey Livoywa Madekwa alisema neno moja pekee, “Mtalii.” Vasiljevic, ambaye aliwasili na mpenzi wake, Marianne anafaa kuwa naibu wa Nikola Kavazovic, ambaye alikuwa kocha mkuu wa Township Rollers nchini Botswana. Hata hivyo, Kavazovic yuko nchini Serbia, huku ripoti zikienea anaviziwa na klabu moja nchini Afrika Kusini.

Baada tu ya Leopards kutangaza kusajili Luvanda kutoka Shule ya Upili ya Chavakali High katika kaunti ya Vihiga kwa kandarasi ya miaka mitatu, mashabiki wamechangamkia usajili huo kwenye mitandao ya kijamii. “Karibu, nitazungumza mengi nikishakuona uwanjani,” amesema Pretold Boge.

Naye shabiki Ignatius Ashibira Shamala hakuridhishwa hata kidogo. Amesema, Tafadhali sajili wachezaji walio na uzoefu…Kwani AFC imekuwa shule ya kukuza vipaji? Inasikitisha.” Oyiengo Benjamin Oduor, “Mnasajili mtoto wa shule ya sekondari? Bure kabisa.”

Naye Dun WA Namale aliashiria kwamba Leopards inakimbilia wachezaji wasiojulikana kwa sababu haina fedha.

“Klabu inaogopa gharama haiwezi lipa kocha ama mchezaji mwenye uzoefu.” Mkenya Ndie Mimi, “Upuzi mtupu… Mbona (Luvanda) asiende akademia kwanza?” Mashabiki wachache sana waliunga mkono afisi ya Leopards kusajili Luvanda wakisema ni mpango mzuri kwa siku za usoni na pia biashara nzuri.

Mabingwa mara 13 Leopards, ambao wanatafuta kushinda ligi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, wataingia mechi ya Sharks wakiwa na rekodi mbaya.

Tangu Sharks iingie katika Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2017, Leopards haijapata ushindi dhidi ya klabu hii inayojivunia ushindi mbili – ikiwemo mara ya mwisho zilikutana Septemba mwaka 2018 – na sare mbili. Leopards imewahi kuchapa Sharks, lakini katika fainali ya soka ya SportPesa Shield mwaka 2017.

Ratiba ya mechi za raundi ya kwanza za Ligi Kuu ya Kenya:

Desemba 8

Mathare United na Chemelil Sugar (Kasarani, 3.00pm)

Bandari na Gor Mahia (Mbaraki, 3.00pm)

Kakamega Homeboyz na KCB (Bukhungu, 3.00pm)

Posta Rangers na Western Stima (Afraha, 3.00pm)

Desemba 9

Mount Kenya United na Sofapaka (Machakos, 2.00pm), Zoo na Nzoia United (Kericho, 3.00pm), SoNy Sugar na Tusker (Awendo, 3.00pm), Vihiga United na Ulinzi Stars (Bukhungu, 3.00pm), AFC Leopards na Kariobangi Sharks (Machakos, 4.15pm).

You can share this post!

Shujaa yakaribishwa Cape Town Sevens kwa kipigo

MSIMU MPYA: Mathare United yaongoza ligi, Gor yajikwaa

adminleo