• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
MSIMU MPYA: Mathare United yaongoza ligi, Gor yajikwaa

MSIMU MPYA: Mathare United yaongoza ligi, Gor yajikwaa

Na GEOFFREY ANENE

Mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United wamechukua uongozi wa mapema wa Ligi Kuu baada ya kusaga Chemelil Sugar 2-0 uwanjani Kasarani, Jumamosi.

Mabao ya Cliff Nyakeya dakika ya tano na Clifford Alwanga dakika ya 13 yalitosha kuzamisha wanasukari wa Chemelil na kuiweka Mathare ya kocha Francis Kimanzi kileleni katika sikua ya kwanza ya msimu 2018-2019.

Bandari ya kocha Bernard Mwalala inashikilia nafasi ya pili baada ya kunyamazisha mabingwa mara 17 Gor Mahia 2-1 kupitia mabao ya William Wadri na David King’atua.

Gor, ambayo bado inatafuta kocha baada ya Muingereza Dylan Kerr kuondoka wiki chache zilizopita baada ya kuiongoza kushinda ligi msimu 2018, ilijiliwaza na bao kutoka kwa sajili mpya Nicholas Kipkirui.

Western Stima, ambayo imerejea Ligi Kuu baada ya kushiriki Ligi ya Daraja ya Pili mwaka 2018 na kuishinda, iko katika nafasi ya tatu pia kwa alama tatu. Wanaumeme hawa walilipua wenyeji wao Posta Rangers 1-0 kupitia bao la Wesley Kemboi lililopatikana katika dakika ya 65. Nafasi ya nne inashikiliwa na Kakamega Homeboyz, ambayo pia ililemea KCB 1-0 mjini Kakamega. KCB ilitemwa kutoka Ligi Kuu mwaka 2015, lakini ikarejea msimu huu baada ya kukamilisha Ligi ya Supa mwaka 2018 katika nafasi ya pili.  Mathare na KCB zilimaliza mechi watu 10 baada ya wachezaji wao kuonyeshwa kadi nyekundu.

Bandari, ambayo ilianzishwa mwaka 1985, haijawahi kushinda Ligi Kuu. Hata hivyo, ni moja ya klabu zilizofanya vyema mismu uliopita. Ilimaliza msimu katika nafasi ya pili nyuma ya Gor. Ushindi wake dhidi ya Gor ni wa pili mfululizo baada ya kuvunja rekodi ya miamba hawa ya kutoshindwa kwa kuizima 2-1 mwezi Agosti.

Mechi tano zitachezwa Jumapili. AFC Leopards itafungua kampeni dhidi ya Kariobangi Sharks uwanjani Machakos saa chache baada ya Mount Kenya United na Sofapaka kutumia uwanja huu. Mabingwa mara 13 Leopards walipoteza mechi nne zilizopita ligini ikiwemo kuchabangwa 3-1 na Sharks mnamo Septemba 18. Ingwe itakuwa ikitafuta kulipiza kisasi dhidi ya washindi wa SportPesa Shield Sharks tayari wameonesha kuimarika hasa baada ya kukung’uta Gor 1-0 katika soka ya KPL Super Cup mnamo Desemba 2. Sharks ina rekodi nzuri dhidi ya Ingwe ya ushindi mbili, sare mbili na kichapo kimoja.

Ratiba ya Desemba 9: Mount Kenya United na Sofapaka (Machakos, 2.00pm), Zoo na Nzoia United (Kericho, 3.00pm), SoNy Sugar na Tusker (Awendo, 3.00pm), Vihiga United na Ulinzi Stars (Bukhungu, 3.00pm), AFC Leopards na Kariobangi Sharks (Machakos, 4.15pm).

You can share this post!

Mashabiki wa Ingwe wakaribisha kocha mpya kwa matusi na...

Salah sasa ni mkali wao EPL baada ya Reds kuitafuna...

adminleo