• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Salah sasa ni mkali wao EPL baada ya Reds kuitafuna Bournemouth

Salah sasa ni mkali wao EPL baada ya Reds kuitafuna Bournemouth

NA GEOFFREY ANENE

Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2017-2018, Mohamed Salah amerukia juu ya jedwali la wafungaji wa mabao kwenye ligi hiyo msimu huu wa 2018-2019 baada ya kuongoza Liverpool kuponda Bournemouth 4-0 Jumamosi.

Mvamizi huyu matata wa Misri amefunga mabao matatu matamu uwanjani Dean Court na kumfikia Mgabon Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal kwa mabao 10. Hata hivyo, Salah yuko juu sasa kwa sababu pia amechangia pasi mbili zaidi ambazo zilimezalisha mabao. Ana pasi nne naye Aubameyang amemegea wenzake pasi mbili ambazo zimefungwa.

Katika mchuano wa kufungua raundi ya 16 msimu huu kati ya Liverpool na Bournemouth, Salah alianzisha maangamizi alipoona lango dakika ya 25. Alionekana kuwa ameotea Roberto Firmino alipovutia kipa Asmir Begovic shuti kali alililopangua vibaya na kumpata Salah aliyelifunga kwa ustadi kwa guu lake hatari la kushoto.

Mwanasoka huyu bora wa Afrika mwaka 2017, ambaye pia yuko katika orodha ya wanaowania tuzo hii ya kifahari mwaka 2018, alipachika bao lake la pili dakika ya 48 akimwacha Begovic hoi michumani.

Bournemouth ilichoma mwiba dakika ya 68 pale Steve Cook alifungia Liverpool bao safi akijaribu kuondosha krosi hatari ndani ya kisanduku. Salah, 26, ambaye ripoti zinadai yumo mbio kujiunga na miamba wa Uhispania Real Madrid, alipata “hat-trick” yake dakika ya 77 baada ya kuabisha safu ya ulinzi ya Bournemouth ikiwa ni pamoja na kuchenga kipa mara mbili kabla ya kufuma wavuni mpira safi.

Ushindi huu ni wa tatu mfululizo wa Liverpool dhidi ya Bournemouth ambayo katika mechi hizi tatu imefungwa jumla ya mabao 11 bila jibu.

Alama hizi tatu zimesaidia Liverpool kurukia juu ya jedwali kwa alama 42. Mabingwa watetezi Manchester City walikuwa juu kwa alama 41 kabla ya Liverpool kushinda.

City itakuwa uwanjani Stamford Bridge kukabiliana na Chelsea katika mechi ambayo vijana wa kocha Pep Guardiola wanahitaji ushindi kupokonya Liverpool uongozi. Klabu za City na Liverpool ndizo hazijashindwa msimu huu ligini.

You can share this post!

MSIMU MPYA: Mathare United yaongoza ligi, Gor yajikwaa

Honolulu Marathon yavutia wakimbiaji 27,000

adminleo