• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Ajabu ya mnyama kula mioyo pekee na kufyonza damu ya kondoo 50

Ajabu ya mnyama kula mioyo pekee na kufyonza damu ya kondoo 50

Na NDUNGU GACHANE

WAKAZI wa vijiji vya Kirembu na Mukangu katika Kaunti ya Murang’a, wanakadiria hasara baada ya mnyama asiyejulikana kushambulia zaidi ya kondoo 50 kwa wiki mbili sasa, na kula mioyo yao pekee kisha kufyonza damu ya mifugo hao.

Mnyama huyo anayeshukiwa kuwa chui amekuwa akiacha mizoga ya mifugo hao zizini. Wanakijiji sasa wanalaumu Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori nchini (KWS) kwa kukosa kuitikia malalamishi yao ili wamtafute mnyama huyo.

Walidai wamekuwa wakipigia shirika hilo simu kwa miezi minne sasa ilhali hakuna hatua iliyochukuliwa kuwaepushia hasara.

Bi Joyce Wanjiru alishtuka alipoamka Jumamosi na kupata kondoo wake wote watatu wakiwa wameangamizwa.

“Nilikuwa nimeenda zizini kukamua ng’ombe wakati nilipopata kondoo wangu waliobaki walikuwa wameuliwa. Damu ilikuwa inavuja shingoni na vifuani mwao lakini hawakuwa na mioyo,” akasema.

Bw Maina Muya ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kirembu, alisema wanakijiji wengi wamelazimika kuweka mifugo wao ndani ya nyumba wakihofia watashambuliwa usiku.

Alilaumu KWS kwa kupuuza malalamishi yao na kusema kama maafisa wangechukua hatu mapema, idadi ya wanyama waliopotezwa na wakazi haingekuwa kubwa ilivyo kwa sasa.

You can share this post!

Serikali kuchunguza kukatika kwa huduma za M-Pesa

Hedimasta pabaya kuzuia wanafunzi kuenda darasa la 8

adminleo