• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Wananchi wote walazimishwe kupiga kura ili kuzima ufisadi – Kiraitu

Wananchi wote walazimishwe kupiga kura ili kuzima ufisadi – Kiraitu

Na DAVID MUCHUI

GAVANA wa Kaunti ya Meru, Kiraitu Murungi, sasa anataka upigaji kura ufanywe kuwa wa lazima kwa watu wote wazima, kama njia moja ya kukabiliana na ufisadi nchini.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Dhidi ya Ufisadi katika Chuo cha Kiufundi cha Meru, Bw Murungi alitaja siasa kama kiini kikuu cha kuongezeka kwa sakata za ufisadi nchini.

Kiongozi huyo pia alitaja kutoshirikiana miongoni mwa mamlaka za kisheria na usalama kama pengo kubwa ambalo limeathiri vita dhidi ya ufisadi.

Bw Murungi alitia saini Muafaka wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Ufisadi alipohudumu kama Waziri wa Haki mnamo 2003.

Hata hivyo, aliisifu Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC), Idara ya Upelelezi (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ushirikiano wao katika juhudi za kukabiliana na ufisadi.

“Fedha zinazotokana na ufisadi hutumiwa na wanasiasa kuwahonga wapigakura. Ikiwa tutakuwa na sheria inayofanya upigaji kura kuwa lazima, wapigakura hawatahitajika kuhongwa. Sheria hiyo inaweza kupunguza ufisadi wa kisiasa maradufu,” akasema Bw Murungi.

Gavana huyo alisema kuwa mtindo wa wakosoaji wa kisiasa kutumia uvumi kuwaharibia sifa wanasiasa zimewafanya baadhi yao kutojali hata wanapokumbwa na madai hayo.

“Kila mtu anayewania wadhifa mkubwa wa kisiasa anapakwa tope kwa kuhusishwa na madai ya ufisadi na mahasimu wake. Ni mkasa kwamba viongozi wa kidini wanaonekana kuwaunga mkono wafisadi, kwani wamekuwa wakiwabariki kama njia ya kujitafutia utajiri. Tunahitaji mfumo mpya wa uongozi wa kidini na utoaji huduma kwa wananchi ambao unakashifu vikali ufisadi,” akasema.

Bw Murungi alisema kuwa serikali yake imeweka mikakati kuhakikisha kwamba imezima mianya yote ya ufisadi ili kuboresha huduma inazotoa kwa umma.

“Nilipochukua uongozi, niliagiza utathmini wa kina wa madeni yaliyoachwa na uongozi uliotangulia. Hilo lilituwezesha kuzuia kupotea kwa Sh900 milioni za umma,” akasema.

Alieleza kuwa kuna haja ya tume ya EACC kuongezwa fedha zaidi ili kuiwezesha kutoa mafunzo kwa Wakenya kuhusu njia za kukabiliana na ufisadi.

Wakati wa hafla hiyo, Naibu Mwenyekiti wa tume hiyo Sophia Lepuchirit aliwaonya magavana dhidi ya kuendeleza ufisadi, akisema kuwa baadhi yao wanachunguzwa kwa kujumuisha jamaa zao kwenye shughuli za utoaji kandarasi kwa kaunti.

“Kila mmoja anapaswa kutusaidia kuuelimisha umma kuhusu athari za kupatikana wakijihusisha katika ufisadi. Miongoni mwa hatua tunazochukua dhidi ya washukiwa ni kufunga akaunti zao za benki na za jamaa zao wa karibu. Idadi ya akaunti tulizofunga inashangaza,” akasema.

Alionya kuwa hawatasita kuwachukulia hatua anayetoa na anayepokea kwani wote ni washiriki.

You can share this post!

Hofu wafanyabiashara wakilipa wahuni kuua washindani wao

Mama ajiteketeza na watoto wake nyumbani

adminleo