• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Jeshi la Misri lasema limeua magaidi 12 katika operesheni

Jeshi la Misri lasema limeua magaidi 12 katika operesheni

Jeshi la Misri likilinda doria. Picha/ AFP

Na MASHIRIKA

CAIRO, MISRI

JESHI la Misri limesema kwamba limewaua watu 12 wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji wa Kiislamu, kwenye operesheni kali dhidi ya makundi ya kigaidi.

Taarifa zilisema kwamba watu wengine zaidi ya 100 walikamatwa. Msako huo ulifanyika katika kisiwa kidogo cha Sinai, viungani mwa Cairo, ambacho kimekuwa kikitumika sana magaidi kutekeleza mashambulio yao.

Aidha, takwimu hizo zilitolewa siku moja baada ya jeshi kuwahi kuwaua wapiganaji wengine 16 kwenye operesheni hiyo.

Jeshi la angani pia lilidai kuyashambulia maeneo 60 ya wapiganaji hao, yakijumuisha magari, mabohari ya silaha na vituo vya mawasiliano. Licha ya takwimu hizo, idadi ya waliojeruhiwa haikubainika mara moja.

Misri ilianza operesheni hiyo kali inayoendeshwa kwa pamoja na jeshi la ardhini, majini na katika hewa kwa lengo la kuyafurusha makundi ya kigaidi katika kisiwa hicho, eneo la Nile Delta na Western Delta.

Makundi yanayolengwa katika operesheni hiyo ni Muslim Brotherhood, Islamic State (IS) na Al-Qaeda.

Hilo linaonekana kusukumwa na mashambulio mabaya ya kigaidi ambayo makundi hayo yamekuwa yakitekeleza.

Mnamo Novemba mwaka uliopita, watu 235 waliuawa kwenye shambulio dhidi ya msikiti mmoja katika mji wa Bir al-Bed, ambapo linaaminika kutekelezwa na kundi la IS.

You can share this post!

Juhudi za kumwondoa Rais Zuma mamlakani zashika kasi

Ufaransa yaahidi kusaidia Iraq kujijenga upya

adminleo