• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
NGILA: Wazo la Silicon Savannah ya Nairobi lifufuliwe

NGILA: Wazo la Silicon Savannah ya Nairobi lifufuliwe

Na FAUSTINE NGILA

KWA mara nyingine tena, Kenya imetambuliwa barani Afrika kwa uvumbuzi wa programu ya simu ambayo imeiletea dunia matumaini katika vita dhidi ya ukeketaji wa wasichana na wanawake.

Nawapongeza wanafunzi watano wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu waliovumbua I-cut, programu ambayo inawapa nafasi wasichana walio katika hatari ya kukeketwa kupiga ripoti kwa maafisa husika na kuokolewa kwa kubonyeza kitufe kwa simu.

Hii ni ithibati ya wazi kuwa, licha ya uvumbuzi wa programu nyingi za simu kutawalwa na wanaume, wanawake wana uwezo sawa wa ubunifu na kuibua teknolojia zinazosaidia jamii kukabiliana na changamoto sugu.

Ingawa wasichana hao watatuzwa Sh2.5 milioni jijini Abuja, Nigeria kwa weledi wao, ni aibu kuu kwa taifa walikozaliwa kuchelewa kuwatambua.

Inasikitisha kukosa kusikia lolote kutoka kwa Wizara ya Afya, Elimu na ile ya Teknolojia ya Mawasiliano, asasi muhimu za serikali ambazo zinastahili kuwa mstari wa mbele katika upigaji jeki wa wananchi wenye akili pevu za kukabili matatizo ya kijamii kupitia teknolojia.

Ukeketaji ni kisiki kikuu katika maendeleo ya mataifa mengi, hasa wanawake kwani tohara hiyo huwaathiri kiakili, kiafya na kimwili na kuwaacha na unyanyapaa na kusababisha na kueneza maradhi kama pepopunda na hatimaye waathiriwa kufariki.

Mbona tusubiri shirika kutoka Nigeria lililoweka miundombinu mwafaka lije kutufunua macho kuhusu uwezo mkubwa ulioko katika vijana wa humu nchini?

Nimesema mara si haba kuwa Kenya ni taifa lililobarikiwa na vijana wabunifu kiteknolojia, ila wanachokosa ni miundomsingi na miundombinu ya kutekeleza mawazo yao na kuzalisha programu za maana.

Ni kweli kuna kituo cha uvumbuzi cha iHub jijini Nairobi lakini kituo kimoja hakitoshi kwa taifa ambalo vijana wake wanatambua mifumo ya kidijitali kama suluhu ya vizingiti vingi maishani.

Serikali kuu ikishirikiana na zile za kaunti zinafaa kuunda angalau kituo kimoja katika kila kaunti, na kutengewa ubunifu, sayansi na teknolojia, iwapo taifa hili kwa kweli litavuna pakubwa kutokana na kasi yake ya juu zaidi ya intaneti hapa barani.

Taifa la Amerika kwa mfano, lilitenga jimbo la California, eneo la Silicon Valley ambako uvumbuzi unaotawala duniani kwa sasa ulianzia. Kampuni tajika kama Google, Facebook, Twitter, LinkedIn, Uber, Apple, Adobe Systems, Cisco, HP, Netflix, Oracle, Tesla, Intel na zinginezo ziliasisiwa hapo.

Wazo la Silicon Savannah ya Nairobi liliyeyukia wapi?

Vipaji vya teknolojia vilivyoko humu nchini vitaozea kwa mienendo duni kama ubashiri wa michezo na kamari licha ya bei ya intaneti kuzidi kupungua, iwapo serikali itazidi kufumbia macho suala hili.

You can share this post!

TAHARIRI: Matokeo mazuri si shule tu bali pia juhudi

ONYANGO: Nia ya kufadhili vyama hivi vya kisiasa haifai

adminleo