• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
ODM kuwania urais 2022 bila kuwajali vinara wa Nasa

ODM kuwania urais 2022 bila kuwajali vinara wa Nasa

SHABAN MAKOKHA na GAITANO PESSA

CHAMA cha ODM kimesema kwamba kitakuwa na mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kwamba hakitaunga vinara wenza wa NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi au Moses Wetangula.

Hata hivyo, Bw Musyoka aliwataka wanasiasa kusitisha siasa za uchaguzi mkuu kwa wakati huu na kuhudumia Wakenya.

Jumanne, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alisema chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, kinalenga kujiimarisha kwa sababu hakijatimiza malengo yake na kwamba kina haki ya kikatiba ya kutoa mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kauli ya Bw Sifuna inaashiria kuwa chama hicho hakithamini tena muungano wa NASA kiliobuni pamoja na chama cha Wiper cha Bw Musyoka, ANC cha Mudavadi na Fork Kenya cha Moses Wetangula .

Akiongea kwenye mahojiano na Radio Citizen Jumatatu asubuhi, Bw Sifuna alisema ODM hakishughuliki na masuala ya NASA akisema muungano huo unadumu katika karatasi pekee kufuatia mkataba uliowasilishwa kwa msajili wa vyama vya kisiasa.

“NASA iliisha Januari 30, 2018 wakati vinara wengine wa muungano huo walikosa kufika Uhuru Park wakati wa kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa rais wa wananchi,” alisema Bw Sifuna.

Bw Sifuna alisema Bw Musyoka, Mudavadi na Wetangula walisaliti Bw Odinga kwa kutohudhuria hafla ya kuapishwa kwake.

“Mwaka wa 2022, tutakuwa na mgombea urais maarufu ambaye atamrithi Rais Kenyatta. Tuko na viongozi wazuri ambao wametangaza azma yao ya kuingia Ikulu 2022,”alisema. Miongoni mwa wanachama wa ODM ambao wana nia ya kugombea urais ni Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakimtaka Bw Odinga kugombea urais kwa mara ya tano.

You can share this post!

Huzuni 3 wakifariki baada ya kufunikwa na mawe timboni

WANDERI: Uhuru na Raila, haki za waliofariki 2017 zi wapi?

adminleo