• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mmoja auawa, washukiwa 10 wa genge hatari wakinaswa Mombasa

Mmoja auawa, washukiwa 10 wa genge hatari wakinaswa Mombasa

Na MOHAMED AHMED

MWANAMUME mmoja aliuawa Jumanne huku wengine wakiachwa na majeraha mabaya baada ya kuvamiwa na genge hatari katika maeneo ya Kisauni na Nyali katika kaunti ya Mombasa.

Matukio hayo ya Jumatatu usiku yalipelekea kukamatwa kwa washukiwa 10 wanaoaminika kuwa wanachama wa genge hilo ambalo limekosesha polisi na wakazi wa maeneo bunge hayo usingizi.

kamanda wa polisi kaunti ya Mombasa Johnston Ipara jana alisema kuwa miongoni mwa washukiwa hao ni pamoja na mwanamke.

Operesheni hiyo iliongozwa na Bw Ipara ilihusisha maafisa zaidi ya 20 pamoja na vijana wa maeneo ya Kadzandani waliokuwa wamechoshwa na uvamizi huo.

Baadhi ya maeneo ambayo mashambulio hayo yamechacha ni pamoja na Kadzandani, Vikwatani, Mafisini, Soweto Junda , Mishomoroni na Kwa Bulo ambapo genge hilo la kutisha limekuwa likiendeleza operesheni zake.

“Leo tumevamia eneo hili baada ya kupata habari kuwa mmoja ya mkuu wa genge hili ambaye tunamsaka alikuwa hapa lakini kwa bahati mbaya aliweza kutoroka na tunamfuatilizia kwani taarifa ambazo zimetoka kwa hao wengine zitatusaidia,” akasema Bw Ipara.

Kilo mita chache na eneo hilo ambalo polisi walikuwa wamevamia ndipo watu watatu kati ya wanne hao walikuwa wamevamiwa na kukatwakatwa na mapanga eneo la Kwa Bulo.

Miongoni mwa waathiriwa hao ni pamoja na mwanamke ambaye anamiliki duka la Mpesa

Mwanamke huyo anauguza majeraha katika hospitali ya Jocham na waathiriwa wengine wawili wauguza majeraha yao katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani.

Wawili hao ni pamoja na Anthony Mutunga na Stanley Mbito ambao wote walipigwa mapanga ya kichwa.

Kulingana na aliyeshuhudia kisa hicho Bw Martin Chunguti alisema kuwa wahalifu hao walikuwa wamejihami kwa bastola na mapanga.

Bw Chunguti ambaye ni mjombake Bw Mutunga alisema kuwa majambazi hao walivamia eneo hilo la Kwa Bulo na kuanza kukatakata watu kwa mapanga bila kujali.

“Walikuwa wanaenda duka moja baada ya jengine pamoja na nyumba na kuamuru watu waingie ndani na baadaye kuvamia wafanyabiashara hao pamoja na mpwa wangu. Matukio haya yamepeleka wakazi kuishi kwa hofu kubwa sana,” akasema Bw Chunguti.

Afisa mkuu wa matibabu katika hospitali ya CPGH Anthony Mogaka alisema kuwa ndani ya siku tatu pekee watu 18 wamepelekwa hospitalini humo kwa kesi za uvamizi uliotekelezwa katika maeneo tofauti ya Mombasa.

“Wengi wao ni kutoka maeneo ya Kisauni na Mishomoroni na huwa waathiriwa hao wamejeruhiwa kichwani. Visa hivi vimezidi mno,” akasema Bw Mogaka.

  • Tags

You can share this post!

Hofu Uganda wakazi wakizidi kutumia ARVs kugema mvinyo

Mkewe bosi atimua kidosho akidai atampokonya mume

adminleo