• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wezi wa pikipiki Pokot Magharibi sasa waotea Probox

Wezi wa pikipiki Pokot Magharibi sasa waotea Probox

Na OSCAR KAKAI

VIONGOZI katika kaunti ya Pokot Magharibi wamelalamikia ongezeko la visa vya wizi wa magari hasa aina ya Probox katika mji wa Kapenguria na viungani mwake.

Awali, eneo hilo lilikuwa likishuhudia wizi mwingi wa pikipiki na sasa umegeuka hadi kwa wizi wa magari ya kibinafsi.

Viongozi hao wametoa wito kwa serikali kuharakisna kutatua shida hiyo kabla haijaenea zaidi.

Naibu wa gavana wa kaunti hiyo Dkt Nicholas Atudonyang na mbunge wa Kapenguria BwSamuel Moroto walidai kuwa maafisa wa usaama wametelekeza majukumu yenye umuhimu na kuwataka wawajibikie suala hilo.

Dkt Atudonyang alisema ni aibu ya maafisa kuendelea kutochukua hatua ilihali wizi wa magari unaongezeka kila siku.

“Wezi hao wanafaa kukoma. Hii ni nchi yetu na hamwezi kuja hapa kuiba. Hatutaki watu kuja hapa kuiba. Maafisa wa usalama hawajatuambia chochote,” alisema.

Bw Moroto alisema kuwa wako na habari kuhusu wezi hao ambao wameibia wakazi magari yao.

“Tumepoteza mali yote. Tunaelewa kile ambacho kinaendelea na hivi karibuni tutafanya msako kuhusu wezi hao. Lazima tukomeshe tabia hii,” alisema Bw Moroto.

Mbunge huyo ambaye alikuwa na gadhabu alisema kuwa ikiwa serikali itashindwa kutatua suala hilo basi yeye pamoja na wakazi watalinda mali yao.

You can share this post!

Wito mataifa yote yafunge biashara ya bidhaa za wanyamapori

Asilimia 80 ya waliokufa ajalini ni wanaume – Ripoti

adminleo