• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Asilimia 80 ya waliokufa ajalini ni wanaume – Ripoti

Asilimia 80 ya waliokufa ajalini ni wanaume – Ripoti

Na COLLINS OMULO

ASILIMIA 80 ya watu 2,922 waliofariki katika ajali za barabarani ni wanaume, kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA).

Ripoti hiyo iliyo na takwimu za ajali kufikia Desemba 10, inaonyesha kuwa wanaume 2,330 walifariki kati ya Januari na mwezi huu ikilinganishwa na wanawake 592 katika kipindi sawa.

Mnamo 2017, wanaume 2,342 walifariki katika ajali za barabarani ikilinganishwa na wanawake 577 ndani ya kipindi sawa. Ripoti inaonyesha kuwa mwezi wa Oktoba ndio ulikuwa hatari zaidi kwani watu 286 waliangamia barabarani.

Oktoba ilifuatiwa na mwezi wa Agosti na Aprili ambapo watu 278 na 269 walifariki katika ajali za barabarani mtawalia.

Miezi ya Septemba, Februari na Julai ilirekodi vifo 266, 257 na 248 mtawalia.

Watu 246 waliangamia barabarani Novemba licha ya kuwepo kwa juhudi za serikali kutekeleza Sheria za Michuki. Idadi hiyo ilizidi ile ya 2017 ambapo watu 240 walifariki barabarani.

Ripoti pia imebaini kuwa jiji la Nairobi linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya barabarani.

Watu 411 walifariki barabarani jijini Nairobi, Kiambu (270), Nakuru (230).

“Majiji ya Mombasa na Kisumu yalirekodi vifo 46 na 96 mtawalia,” inasema ripoti.

Watu 178, 124 na 124 waliangamia katika Kaunti za Machakos, Kericho na Makueni mtawalia.

Kaunti za Elgeyo Marakwet, Tharaka Nithi, Isiolo, Mandera, Wajir na Marsabit zilirekodi vifo 4, 8, 9, 9, 10 na 10 mtawalia. Magari ya kibinafsi yanaongoza katika kusababisha ajali.

“Watu 756 waliofariki katika ajali za barabarani walikuwa katika magari ya kibinafsi. Magari ya kibiashara kama vile malori yalisababisha vifo vya watu 672 na magari ya usafiri wa umma vifo 570,” inasema ripoti ya NTSA.

Pikipiki zinafuatia kwa karibu kwa kusababisha vifo 486 na watu 373 waendao kwa miguu waliogongwa na kufa na magari yaliyotoweka baadaye.

Magari ya serikali yaliua watu 37, magari yenye gurudumu tatu kama vile tuktuk yalisababisha vifo vya watu 10, baiskeli vifo 11 na mikokoteni iliua mtu mmoja.

Watu 1,117 waendao kwa miguu waligongwa na kufaa na vyombo mbalimbali vya usafiri.

Mwaka jana watu 999 waendao kwa miguu waligongwa na kufariki katika kipindi sawa.

Bodaboda zilisababisha vifo 775 mwaka huu ikilinganishwa na 674, mwaka uliopita.

Abiria wa magari 682 wakiaga dunia tangu Januari ikilinganishwa na 650 katika kipindi sawa mwaka jana.

Idadi ya madereva waliofariki katika ajali za barabarani ilipungua kwa kiasi kidogo hadi 285 mwaka huu ikilinganishwa na 290 katika kipindi sawa mwaka jana.

You can share this post!

Wezi wa pikipiki Pokot Magharibi sasa waotea Probox

EACC: Bunge kuamua ikiwa Mbarak anafaa kuongoza tume

adminleo