• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Maandalizi ya Stars U-20 yakosa kung’oa nanga tena

Maandalizi ya Stars U-20 yakosa kung’oa nanga tena

Kiongozi wa makocha wanaohusika katika utafutaji wa vijana wanaojivunia utajiri wa vipaji kwa minajili ya kikosi hicho cha Rising Stars, Stanley Okumbi. Picha/Maktaba

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari:

  • Chipukizi hao walitarajiwa kuingia kambini katika uwanja wa kimataifa wa MISC Kasarani mnamo Februari 5, 2018
  • Okumbi amekuwa akitumia mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom kutambua makinda wenye uwezo 
  • Ziara ya kutafuta tiketi ya kuelekea nchini Niger mnamo 2019 kwa Kombe la AFCON inatarajiwa kuanza mapema Aprili 2018
  • Okumbi amesalia katika benchi la kiufundi la Harambee Stars licha ya kuvuliwa wadhifa wa kocha mkuu

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 (Under-20) ilikosa kuanza Jumanne , maandalizi yake kwa minajili ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kama ilivyopangwa awali.

Ni mara ya pili kwa maandalizi ya kikosi hicho kuchelewa kuanza licha ya ugumu na uzito wa kibarua kilichopo mbele ya vijana hao almaarufu Harambee Rising Stars.

Chipukizi hao walitarajiwa kuingia kambini katika uwanja wa kimataifa wa MISC Kasarani mnamo Februari 5, 2018 lakini shughuli za kuwasaka wachezaji wa kuunga na kukamilisha kikosi chenyewe hazikuwa zimekamilika.

Kiongozi wa makocha wanaohusika katika utafutaji wa vijana wanaojivunia utajiri wa vipaji kwa minajili ya kikosi hicho cha Rising Stars, Stanley Okumbi alisema Jumanne kwamba wako katika hatua za mwisho za kukamilisha kuunga orodha ya mwisho ya wachezaji watakaopeperusha bendera ya Kenya katika michuano hiyo.

 

Mkutano

Hata hivyo, Okumbi alisisitiza kwamba majina ya wachezaji na tarehe ya kuanza rasmi kwa mazoezi itatolewa na wadau husika baada ya kuandaliwa kwa mkutano muhimu mnamo Alhamisi.

Okumbi ambaye sasa ni kocha msaidizi wa Harambee Stars baada ya Mbelgiji Paul Put kurithi mikoba yake, amekuwa akitumia mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom kutambua makinda wenye uwezo wa kukitambisha kikosi cha Rising Stars katika kampeni hizo za kimataifa.

Isitoshe, alidokeza uwezekano wa kuzihemea pia huduma za chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20 katika klabu mbalimbali za humu nchini.

Rising Stars imeratibiwa kuvaana na Tanzania katika mechi ya kirafiki mnamo Machi 3, 2018 jijini Dar es Salaam. Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) pia lilianika majuzi maazimio ya kuwajumuisha Rising Stars katika mashindano ya mataifa manne yatakayoandaliwa nchini Misri mapema mwezi Machi.

 

Aprili

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) bado halijafanya droo wala kutangaza tarehe rasmi za kupigwa kwa mechi za mchujo, lakini ziara ya kutafuta tiketi ya kuelekea nchini Niger mnamo 2019 kwa minajili ya Kombe la AFCON inatarajiwa kuanza mapema Aprili 2018.

“Tunanuia kutumia mchuano wa kupimana nguvu utakaotukutanisha na Tanzania ili kuwapa vijana uzoefu wa kutandaza soka hiyo katika kiwango cha kimataifa wakati wanapojiandaa kwa msururu wa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika,” akasema Afisa Mkuu wa FKF, Robert Muthomi kwa kukiri kwamba kipute cha Chapa Dimba Na Safaricom kiliwapa jukwaa mwafaka la kutambua vijana wenye uwezo mkubwa katika ulingo wa soka.

Kenya haijawahi kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 tangu 1981.

Katika juhudi za kuwania tiketi ya kushiriki mapambano hayo mnamo 2007, vijana wa nyumbani waliwakomoa Djibouti 1-0 katika awamu ya mchujo kabla ya kubanduliwa na Rwanda kwenye raundi ya kwanza baada ya kuzidiwa maarifa katika mechi za mikondo miwili iliyotandazwa jijini Nairobi na Kigali.

 

Kubanduliwa na Sudan, Lesotho na Misri 

Katika jaribio jingine mnamo 2009, Kenya walilambishwa sakafu na Sudan katika raundi ya kwanza licha ya kuwapepeta Somalia katika michuano ya michujo.

Miaka miwili baadaye, chipukizi hao waling’olewa na Lesotho waliowapokeza kichapo cha 1-0 katika mechi ya marudiano baada ya kusajili sare tasa katika kivumbi cha mkondo wa kwanza.

Awali mwaka huo, Stars walikuwa wamedumisha uhai wao wa kufuzu kwa fainali za 2011 baada ya wapinzani wao, Eritrea kujiondoa kisha kufanikiwa kuwatandika Sudan kwa jumla ya mabao 3-0 katika raundi ya kwanza.

Mnamo 2013, Kenya walidhalilishwa 3-0 na Misri ambao waliwabandua kwenye raundi ya kwanza ya michuano ya kufuzu kwa fainali za kipute hicho ambacho huandaliwa kila baada ya miaka miwili.

Okumbi alisalia katika benchi la kiufundi la Harambee Stars licha ya kuvuliwa wadhifa wa kocha mkuu na Mbelgiji Paul Put ambaye kwa sasa anahemewa na Guinea kupokezwa mikoba ya kikosi hicho cha taifa mwishoni mwa 2017.

Mabadiliko hayo katika kikosi cha Stars yalichochewa na matokeo duni yaliyosajiliwa na vijana wa taifa katika michuano miwili ya kirafiki dhidi ya Iraq na Thailand mwanzoni mwa Oktoba 2017 chini ya Okumbi ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Mathare United waliotawazwa wafalme wa KPL mnamo 2008 chini ya kocha wao wa sasa, Francis Kimanzi.

 

You can share this post!

Droo ya KPL Top 8 sasa ni hadi Machi

ANC sasa yamkabidhi Rais Zuma barua rasmi ya kumtaka...

adminleo