• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
KAULI YA WALIBORA: Tukumbatie wingilugha ili kukabili changamoto za kimawasiliano

KAULI YA WALIBORA: Tukumbatie wingilugha ili kukabili changamoto za kimawasiliano

NA PROF KEN WALIBORA

Sikujua tija ya wingilugha hadi nilipozuru Senegal kwa mara ya pili mwezi huu unaofunga mwaka wa 2018.

Mwaliko wa kuhudhuria na kuwasilisha mada katika kongomano la Baraza la Ukuzaji Utafiti wa Sayansi za Jamii barani Afrika (CODESRIA) umenifikisha katika nchi ya mwanafalsafa na kiongozi wa Kiafrika Leopold Senghor kwa mara ya pili maishani mwangu.

Mara ya kwanza kuzuru Senegal ulikuwa mwaka 2015. Katika kongomano la kwanza sikuwasilisha, nilikuwa mtazamaji, au niseme nilikuwa mwanahabari aliyeshuhudia wasomi wenzangu wakila uhondo wa taaluma. Safari hii hata mimi nimo.

Nilikuwa katika rubaa ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika waliowasili Jumapili jioni katika uwanja wa jiji kuu la Senegal Dakar. Punde tulilakiwa na wenyeji wetu na wengi wao hawazungumzi Kiswahili wala Kiingereza.

Wao ni weledi wa Kiwolof na Kifaransa, hasa dereva wa basi lililotutoa uwanja wa ndege mpaka katikati ya jiji. Nilikaa mbele na dereva ili nione vizuri mandhari ya nchi hii ya Sadio Mane wa Liverpool.

Nikimuuliza swali dereva kwa Kiingereza ananijibu kwa Kifaransa au Kiwolof. Potelea pote, nikaamua kusema naye Kiswahili! Hata siku moja sijawazia kufanya kazi ya kuchekesha watu, (au uchale), lakini unaweza kukisia jinsi abiria wote garini walivyoangua kicheko, hata dereva mwenyewe.

Yaani kumbe hiki Kiswahili tunakijua na kukienzi lakini mara nyingine kinachekesha tu, hakiwezeshi mawasiliano kila pahali na kwa kila mtu. Kiswahili changu kilikuwa kikwazo kwa mawasiliano na dereva ambaye labda ni mtu wa nasaba ya Alhajj Diouf, mchezaji wa zamani wa Liverpool. Naye kashindwa kufanikisha mawasiliano kwa Kiwolof au Kifaransa chake.

Ndipo alipotokea ndugu yetu mmoja msomi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akaokoa jahazi. Msomi huyo alikuwa mweledi wa Kifaransa cha dereva na Kiswahili changu.

Mara moja akalitwaa jukumu la kuwa mkalimani na kuwezesha mawasilino kati yangu na dereva wetu. Ndipo wiki hii niliamua sharti niandike kuhusu wingilugha, yaani kuwapo na lugha nyingi au mtu kuwa na umilisi wa lugha nyingi. Nawazia ndugu yetu Mkongo anayezungumza Kilingala, Kifaransa, Kiswahili na Kiingereza.

Baadaye kongomano lilipoanza, tulijulishwa kwa msomi mmoja anayezungumza Kibambara, Kihausa, Kiarabu, Kifaransa, Kiiingereza na lugha nyingine nyingi. Sote wajumbe katika kongomano tuliachama kwa hilo na kumshangilia msomi huyu si haba.

Usicheze watu wana vipaji ati. Na hata kwetu Afrika Mashariki kuna watu wenye vipaji vya kujua lugha nyingi. Mfano mtangazaji wa mpira Benardo Otieno niliyewahi kufanya naye kazi KBC na NTV, ambaye alikijua Kijaluo, Kiingereza, Kikamba, Kifaransa, Kijerumani, Kitaliano, Kikikuyu na lugha nyingine nyingi. Wengine ni msanii na mwanahabari Lolani Kalu na marehemu rafiki yangu Omar Babu maarufu kwa Abu Marjan.

Nawahusudu hawa. Tukipende Kiswahili na hata tuwe tayari kukifia ikibidi, lakini tusiachwe tupitwe na umuhimu wa wingilugha.

You can share this post!

TAHARIRI: TSC na Wizara ya Elimu zimalize tofauti zao

Kikosi cha Gor kitakacholimana na Lobi Stars ya Nigeria 

adminleo