• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Wanahabari huru kuangazia kesi ya ufisadi inayokabili Kenya Power

Wanahabari huru kuangazia kesi ya ufisadi inayokabili Kenya Power

Na RICHARD MUNGUTI

JARIBIO la Mkurugenzi wa Uchunguzi (DCI) wa Jinai kuzima vyombo vya habari kuchapisha habari kuhusu kesi ya ununuzi wa transfoma feki zilizopelekea kampuni ya Kenya Power kupoteza zaidi ya Sh408milioni jana liligonga mwamba.

DCI kupitia kwa naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bw Alexander aliomba mahakama iwachukulie hatua wanahabari kwa kuchapisha habari alizodai zinapotosha kuhusu ununuzi wa transfoma hizo.

Bw Muteti alimsihi hakimu azime vyombo vya habari kuchapisha taarifa jinsi kesi hiyo inavyoendelea.

Lakini hakimu mwandamizi mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Felix Kombo alitupilia mbali ombi hilo akisema vyombo vya habari vinatekeleza wajibu muhimu kuwaelimisha wananchi jinsi pesa za umma zinavyotumika.

Bw Kombo alisema vyombo vya habari vimekuwa katika msitari wa mbele kuangazia masuala mbali mbali kuhusu utendakazi serikalini.

“Nimezisoma habari zilizochapishwa Jumatatu na Jumanne na Magazeti ya Nation Media Group na Standard Group kuhusu ushahidi uliotolewa na mashahidi na taarifa ya utangulizi ya Bw Muteti. Hakuna makosa yoyote yaliyotokea kutokana na habari hizo,” alisema Bw Kombo.

Aliongeza kusema kuwa itabidi DCI na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wajue wakifanya kazi duni bila shaka itaangaziwa jinsi ilivyo na wanahabri.

“Itabidi DCI na DPP wavumilie jinsi habari zinavyopeperushwa kwa vile hazina upotovu wowote.Ziko sawa kabisa. Heko wanahabari kwa kunakili ushahidi jinsi ulivyokuwa,” alisema Bw Kombo.

Hakimu aliendelea kusema , “Wanahabari walionukuu ushahidi hawakukosea hata kidogo. Habari zilizochapishwa zinaambatana na rekodi niliyoandika na ushahidi jinsi ulivyotolewa na Bw Linus Ndege Muriithi.”

Akihojiwa na mawakili wanaowatetea washtakiwa Bw Ndege alikiri aliandikia ripoti kuhusu transfoma hizo katika afisi ya DCI kinyume na vile alikuwa amesema hapo mbeleni.

Kombo alisema shahidi huyo alieleza kwa undani jinsi alivyoamriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ununuzi wa bidhaa zinazotumiwa na sekta ya umma na mashirika ya serikali Bw Morris Juma azindue uchunguzi kuhusu ununuzi wa transfoma uliotekelezwa na kampuni ya Muwa Trading Company.

Hakimu alisema Bw Muriithi alieleza uchunguzi aliofanya ulifichua jinsi waliokuwa wakuu wa KP Dkt Ben Chumo , Dkt Ken Tarus na washukiwa wengine 13 walivyokataa kufuata sheria katika ununuzi wa transfoma zaidi ya 300.

Bw Muriithi alieleza korti kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi wake alimrudishia Bw Juma ripoti hiyo.

“Nilimkabidhi Bw Juma ripoti hiyo iliyopelekewa DCI kupitia kwa afisa ajulikanaye kwa jina Nyawinda,” alisema Bw Muriithi.

Mahakama ilielezwa kuwa sheria zilivunjwa na transfoma duni zikanunuliwa na kuwekwa katika yadi ya KP.

Pia korti ilifahamishwa kampuni zilizohusishwa zililipwa zaidi ya Sh6.1 bilioni.

Transfoma zilizonunuliwa na Muwa zilirudishwa ng’ambo zilikonunuliwa kisha ikaishtaki KP na kulipwa mamilioni ya pesa.

Dkt Chumo na wenzake wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.

You can share this post!

Mwanafunzi amtetea mwalimu kwenye kesi ya unajisi

Joho kuwaajiri waliopata ‘first class’ Chuo...

adminleo