• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Naibu Rais sasa kuitwa Dkt William Ruto

Naibu Rais sasa kuitwa Dkt William Ruto

Na PETER MBURU

NAIBU wa Rais William Ruto kuanzia Ijumaa ataitwa daktari, baada ya kupokezwa cheti cha uzamifu (PhD) na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) wakati wa hafla ya kufuzu kwa mahafala, kufuatia miaka sita ya kusomea shahada ya uzamifu.

Dkt Ruto alipokezwa cheti hicho Ijumaa  na Chansela wa UoN Dkt Vijoo Rattansi mbele ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Bw Ruto tangu 2012 amekuwa akisomea PhD katika masuala ya mimea na mazingira yake (plant ecology) hadi alipoidhinishwa kuwa amefuzu, mwisho wa mwezi Novemba.

Na kama furaha juu ya nyingine, siku hii inaafikiana na ile aliyozaliwa na pia ile aliyofunga ndoa na mkewe Rachel.

Kiongozi huyo leo, Desemba 21 anafikisha miaka 52 tangu alipozaliwa mnamo 1966 na pia anafikisha miaka 27 tangu alipofunga pingu za maisha mnamo 1991.

Aliwasilisha utafiti wake wa mwisho kuhusu athari za vitendo vya binadamu kwa matumizi ya ardhi na mazingira kwa maeneo yenye unyevu baada ya kutafiti Saiwa Swamp eneo la magharibi mwa Kenya mnamo Septemba mwaka huu.

Hii ilikuwa miaka sita baada ya utafiti wake kuidhinishwa mnamo Agosti 2012. Aliwasilisha utafiti huo mbele ya wahadhiri mnamo Oktoba 2 na ukaruhusiwa siku iliyofuata.

Naibu wa Rais aidha ana shahada katika masomo ya mimea na wanyama kutoka chuo hicho cha Nairobi ambapo alifuzu mnamo 1990 na shahada ya uzamili kuhusu Plant Ecology, ambayo alipata mnamo 2011.

Alianzia masomo yake ya awali katika shule ya msingi ya Kerotet, akajiunga na shule ya upili ya Wareng kisha ya Kapsabet Boys, eneo la Nandi Hills.

Bw Ruto alipaswa kufuzu na shahada hii ya PhD miaka miwili iliyopita lakini akafeli mtihani.

“Nashauri vyuo vyote kuzingatia viwango vinavyofaa kutoa vyeti kwa wanafunzi ili iwe wale wanaofaa. Kama mwanafunzi wa PhD, nilifaa kufuzu lakini siwezi kwani sijafikia viwango,” alisema wakati huo.

Tangu wakati huo amekuwa mbioni kukimbizana na masuala ya masomo, nyakati zingie akichelewa ama kuahirisha mikutano ya serikali ili kutimiza matakwa ya wasimamizi wake.

Mnamo 2016, Bw Ruto alikosolewa vikubwa baada ya kuvalia vazi la mahafala wa shahada ya PhD alipokuwa mgeni mashuhuri katika hafla ya kufuzu kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Daystar, akiambiwa kuwa amevuka mipaka ya kielimu.

Hii ilikuwa kwa kuwa mtu haruhusiwi kuvalia vazi hilo wakati hajafuzu na shahada ya Uzamifu.

Hii leo, naibu wa Rais ataungana na wanafunzi wengine 9,000 wa chuo cha UoN kufuzu katika sherehe iliyopangwa kuanza asubuhi.

Watu wengine mashuhuri watakaofuzu pamoja naye ni naibu wa Jaji Mkuu Philomena Mwilu, waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa na seneta wa Meru Mithika Linturi ambao wanapokea shahada za uzamili katika sheria.

Takwimu katika wizara ya elimu zinaonyesha kuwa Kenya ina chini ya watu 10,000 ambao wana shahada za PhD, huku mwaka uliopita ni wanafunzi 369 pekee ambao walifuzu na shahada hiyo nchini.

You can share this post!

Makasisi wa ACK waliofutwa kulipwa Sh6.8 milioni

Sonko abomoa vyoo, atisha kubomoa hoteli ya Marble Arch

adminleo