• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Mamangu alinipa kiamsha kinywa cha busaa kila siku, asimulia chifu

Mamangu alinipa kiamsha kinywa cha busaa kila siku, asimulia chifu

Na MAGDALENE WANJA

WAKENYA wengi wanamkumbuka kama chifu aliyehudhuria mkutano wa rais akiwa mlevi chakari mnamo mwaka wa 2016.

Naibu wa chifu Joseph Wycliffe Rotich wa lokesheni ndogo ya Mawingu katika kaunti ya Nakuru alinaswa na kamera akifoka na kuyumbayumba katika mkutano huo uliokuwa umehudhuriwa na maafisa wakuu serikalini.

Kisa hicho kiligonga vichwa vya habari nchini huku wengi wakishangaa jinsi afisa huyo wa serikali alikosa maadili.

Hata hivyo hii haikuwa mara kwanza Bw Rotich alikuwa najihusisha na ulevi wa kupindukia na yalikuwa ni mazoea.

Aidha, miaka mitatu baadaye, Bw Rotich amebadilika baada ya kufanyiwa marekebisho ya mienendo.

Taifa leo Dijitali ilipomtembelea ofisini mwake baada ya Krismasi, alisimulia jinsi alipatwa na wakati mgumu kukabiliana na tatizo la ulevi tangu utotoni.

“Nilipozaliwa na kulelewa, mamangu alifanya biashara ya kupika na kuuza pombe kama vile chang’aa na busaa. Mara nyingi tulibugia busaa kama kiamsha kinywa na matibabu ya homa,” akasema Bw Rotich.

Vilevile babake alikuwa akimtuma dukani kumnunulia sigara, tabia ambayo ilimfanya kuanza kuvuta sigara akiwa mtoto mdogo.

“Nilipotumwa dukani kumletea babangu sigara, ninimletea na kuzificha zingine ambazo nilivuta mimi,” aliongeza Bw Rotich.

Hii iliendelea hadi alipokuwa shule ya upili ambapo alianza kutumia baadhi ya dawa za kulevya.

Hii iliendelea hata alipokamilisha masomo yake na hata alipopata kazi ya unaibu wa chifu.

“Niliendelea na unywaji wa pombe kupindukia na mara nyingi nilienda nyumbani wakati wa usiku wa manane ,” alisema Bw Rotich.

Mwaka 2016, Rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa kuhudhuria mkutano katika eneo la Molo ila Bw Rotich hakupata habari hiyo.

“Kabla ya siku hiyo, nilikuwa nimeenda kujiburudisha katika eneo la kawaida na kwa sababu sikutaka kusumbuliwa, niliizima simu yangu,” akasema.

Kesho yake asubuhi, Bw Rotich alipoamka alipata ujumbe kuhusu mkutano wa rais na hakuwa na budi kuhudhuria.

 

‘Kuwa macho’

Aliamua kuibeba pombe kwenye chupa ya maji huku akijiambia kuwa ingemsaidia kuwa macho wakati wa mkutano huo.

“Sikujua kuwa mambo yangeharibika zaidi, hali yangu ilikuwa mbaya na nilikuwa sijielewi. Baadhi ya watu walinipiga picha huku wengine wakirekodi video,” alisema Bw Rotich.

Baada ya siku hiyo aliamrishwa kufika katika ofisi kuu za maeneo ambako aliambiwa kuwa kazi yake imekwisha.

Alirejea nyumbani kwake ambako aliishi kwa aibu kwa video hiyo ilikuwa imesambaa sana mitandaoni.

“Siku chache baadaye, aliyekuwa mwenyekiti wa shirika la kukabiliana na mihadarati Nacada Bw John Mututho alinichukua na kunipeleka katika kituo cha marekebisho,” aliongeza Bw Rotich.

Alipelekwa katika hospitali ya Mathari Nairobi ambapo alitibiwa kabla ya kupelekwa kwenye kituo tofauti ambako alikaa kwa muda wa siku 53.

“Katika muda niliokaa katika kituo hicho, nilijiunga na kikundi cha watu waliokuwa wanapitia changamoto sawa na yangu na kufikia leo tunasaidiana katika mawaidha ya jinsi ya kutorudia hali ya hapo hawali,” aliongeza Bw Rotich.

Baada ya marekebisho, chifu huyo alirejeshwa kazini na sasa amejihusisha katika kampeni za kupigana na pombe haramu katika lokesheni yake.

Naibu huyu wa chifu huyo anajihusisha katika mikutano ambapo huwapa ushauri vijana kuhusu madhara ya pombe haramu na mihadarati.

“Jamii yangu inafurahia mabadiliko hayo zaidi haswa mke wangu ambaye alinivumilia kwa zaidi ya muongo mmoja,” alisema Bw Rotich.

You can share this post!

KRISMASI: Polo aliyedai ameenda kesha atiwa adabu na kisura...

Kilio katika ngome za Uhuru na Raila

adminleo