• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Hatuna nia ya kutwaa bandari ya Mombasa, China sasa yasema

Hatuna nia ya kutwaa bandari ya Mombasa, China sasa yasema

Na EDWIN OKOTH

SERIKALI ya China imekanusha kuorodhesha Bandari ya Mombasa kama dhamana ya kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa nchini (SGR).

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa China, Hua Chunying katika taarifa, alisema wasiwasi kwamba Bandari ya Mombasa itatwaliwa na China ikiwa Kenya haitakuwa na uwezo wa kulipa deni la Sh327 bilioni zilizotolewa kama mkopo wa SGR kati ya Mombasa na Nairobi hauna ukweli wowote.

Ripoti iliyotolewa kutoka afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilionyesha kuwa mnamo 2013, serikali ilitumia bandari hiyo kama dhamana ili kupata mkopo kutoka China kujenga reli hiyo.

“Tumechunguza shirika la kifedha husika na kupata madai kuwa serikali ya Kenya ilitumia Bandari ya Mombasa kama dhamana kupata mkopo kufadhili ujenzi wa reli kati ya Mombasa na Nairobi sio ya kweli,” alisema Bw Chunying katika taarifa hiyo ya Desemba 25.

Ripoti hiyo ambayo haikukataliwa au kukubaliwa na mchunguzi mkuu wa hesabu za serikali Edward Ouko ilizua hofu kwamba huenda bandari hiyo, ambayo ni muhimu sana kwa Kenya, huenda ikatwaliwa ikiwa serikali itashindwa kulipa mkopo huo.

Wachunguzi walipata kuwa mali ya KPA ilitumiwa kama dhamana ya mkopo huo wa Sh327 bilioni ambazo China ilikopesha Kenya mnamo 2014.

Wizara ya Uchukuzi, Hazina ya Fedha na Ikulu zinaaminika kuhusika katika mkataba huo, ambao uliidhinishwa wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozuru mjini Beijing, China.

“Mali ya KPA ni wazi kutokana na kuwa ilitia sahihi mkataba huo, ambamo ilitajwa kama mkopaji katika kifungu cha 17.5, kesi yoyote dhidi ya mali yake na mkopeshaji haina ulinzi kwa sababu serikali iliondoa kinga kwake baada ya kutia sahihi mkataba huo,” ilisema barua hiyo ya uchunguzi ya Novemba 16 iliyoandikiwa usimamizi wa KPA.

KPA ilipokea mapato ya Sh42.7 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2016/2017, ukuaji wa asilimia 7.9 ikilinganishwa na mwaka wa kifedha uliotangulia, kulingana na ripoti yake ya kifedha ya hivi punde.

You can share this post!

Wanahabari wavamiwa kwenye kesi ya aliyebaka mtoto wa waziri

Amuua mkewe kwa kununua viatu vya Krismasi bila kumjulisha

adminleo