• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Rashford kinda matata mwenye guu la almasi

Rashford kinda matata mwenye guu la almasi

Na CHRIS ADUNGO

MARCUS Rashford, 21, ni fowadi chipukizi mzawa wa Uingereza ambaye kwa sasa anazidi kuwa tegemeo kubwa kambini mwa Manchester United.

Akiwa mchezaji wa Man-United tangu akiwa kitoto cha umri wa miaka saba pekee, Rashford aliwafungia waajiri wake mabao muhimu katika michuano yake miwili ya kwanza katika kikosi cha kwanza cha miamba hao wa soka ya Uingereza.

Goli lake la kwanza lilikuwa katika Ligi ya Uropa baada ya kujaza pengo la Anthony Martial aliyepata jeraha akipasha misuli moto.

Rashford alipachika wavuni bao lake la pili akivalia jezi za Man-United katika mechi ya Ligi Kuu ya EPL iliyowakutanisha na Arsenal mnamo Februari 2016. Alifunga goli jingine katika gozi lake la kwanza dhidi ya Manchester City kabla ya kutikisa nyavu kwa mara nyingine katika mchuano wake wa kwanza wa League Cup na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Katika kibarua kilichokuwa chake cha kwanza ndani ya jezi ya timu ya taifa, Rashford alitikisa nyavu mnamo Mei 2016 na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufungia Uingereza bao katika mchuano wake wa kwanza wa haiba kubwa ndani ya kikosi cha kwanza.

Akiwa mzawa wa mji wa Wythenshawe, Rashford alianza kupiga soka akivalia jezi za kikosi cha Fletcher Moss Rangers akiwa kinda wa umri wa miaka mitano. Miaka miwili baadaye, alijiunga na academia ya Man-United.

Alikua akimfahamu aliyekuwa mvamizi matata wa Brazil, Ronaldo kuwa kielelezo chake kikuu. Katika mchuano wake wa kwanza kutazama, Rashford alimshuhudia Ronaldo akipachika wavuni mabao matatu dhidi ya Man-United uwanjani Old Trafford mnamo 2003. Mwishoni kwa kipute hicho, Ronaldo alipigiwa saluti na mashabiki wa pande zote wakati akiondoka ugani.

Rashford alipangwa katika kikosi cha akiba cha Man-United kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 21, 2015. Ulikuwa ni mpango wa kocha Louis van Gaal kumwajibisha katika kipindi cha pili katika mchuano wa EPL uliowashuhudia Man-United wakiwapokeza Watford kichapo cha 2-1.

Mnamo Februari 25, 2016, alijaza nafasi ya Martial katika mchuano wa Ligi ya Uropa dhidi ya Midtjylland na akafunga mabao mawili yaliyowasaidia waajiri wake kusajili ushindi mnono wa 5-1 uwanjani Old Trafford.

Magoli hayo yalimweka katika mabuku ya historia kwa kuwa kinda wa kwanza wa umri mdogo zaidi baada ya George Best kufungia Man-United bao katika kampeni za soka ya bara Ulaya.

Siku tatu baadaye, alifunga tena magoli matatu na kuchangia latatu katika ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Man-United katika mechi ya EPL dhidi ya Arsenal uwanjani Old Trafford.

Ufanisi huo ulimfanya kuwa chipukizi wa tatu baada ya Federico Macheda na Danny Welbeck kuwafungia Man-United katika mchuano wa kwanza wa EPL.

Mnamo Machi 2016, Rashford alifunga bao la pekee lililowawezesha kusajili ushindi wa kwanza dhidi ya Man-City katika EPL tangu 2012. Akiwa na umri wa miaka 18 na siku 141, Rashford aliweka historia ya kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kuwafungia Man-United katika gozi la EPL dhidi ya watani wao wa tangu jadi, Man-City.

Bao la dakika za mwisho alilowafungia waajiri wake dhidi ya West Ham United mnamo Aprili 13, 2016 liliwasaidia Man-United kufuzu kwa nusu-fainali za Kombe la FA.

Akiongoza safu ya uvamizi ya Man-United dhidi ya Crystal Palace msimu huo, Rashford alifunga bao na kuwachochea waajiri wake kusajili ushindi wa 2-1 uliowavunia Kombe lao la 12 la FA na taji la kwanza la Rashford akivalia jezi za miamba hao wa soka ya Uingereza.

Licha ya kuanza kupangwa katika kikosi cha kwanza mnamo Februari, alikamilisha kampeni za msimu akijivunia kapuni mabao manane kutokana na michuano 18.

Ufanisi huo ulimfanya atawazwe Chipukizi Bora wa Mwaka katika soka ya EPL. Ilikuwa hadi Mei 30, ambapo Rashford alitia saini mktaba mpya na Man-United katika maelewano yaliyotarajiwa kumdumisha ugani Old Trafford hadi 2020.

Baada ya kudhihirisha ukubwa na upekee wa uwezo wake akivalia jezi za Man-United, kocha Roy Hodgson alimpanga Rashford katika kikosi cha Uingereza kilichoshiriki fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa.

Mnamo Mei 27, alifunga bao dhidi ya Australia kirafiki na kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi nyuma ya Tommy Lawton (1938) kutikisa nyavu za wapinzani katika mchuano wake wa kwanza wa kimataifa.

Akiwa na umri wa miaka 18 na siku 229, alitokea benchi mnamo Juni 16, 2016 kujaza pengo la Adam Lallana katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Wales. Tukio hilo lilimfanya kuvunja rekodi ya Wayne Rooney (2004) na kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kuvalia jezi za Uingereza katika kampeni za Euro.

Kwa miaka miwili iliyopita, Rashford amekuwa akitoka kimapenzi na kichuna Lucia Loi, 20. Hata hivyo, uhusiano wao uliyumbishwa mnamo Mei mwaka huu baada ya kipusa Lauryn Goodman, 27, kukiri kwamba amekuwa katika uhusiano wa siri na Rashford tangu mwishoni mwa 2017.

You can share this post!

Ilivyo, Liverpool hawana mshindani katika EPL na taji la...

Liverpool hawakamatiki baada ya kuitia adabu Arsenal

adminleo