• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
LAPSSET: Ujenzi wa bandari ya Lamu ulivyoboresha maisha ya polisi

LAPSSET: Ujenzi wa bandari ya Lamu ulivyoboresha maisha ya polisi

NA KALUME KAZUNGU

UJENZI unaoendelea wa Mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) katika eneo la Kililana, Kaunti ya Lamu umesaidia pakubwa kuboresha maisha ya maafisa wa usalama wanaohudumu eneo hilo.

Kabla ya mradi huo wa gharama ya Sh 2.5 trilioni kuanza kujengwa, maafisa wa usalama waliokuwa wakipelekwa kuhudumia eneo hilo walijihisi kana kwamba wameonewa, kudhalilishwa, kutelekezwa na kutengwa na wakubwa wao kutokana na hali ngumu ya maisha iliyokuwepo eneo hilo.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, maafisa wa polisi kwenye kituo cha polisi cha LAPSSET kilichoko Kililana wamekuwa wakiishi kwa shida kwenye mahema ambayo yalikuwa yamewekwa  eneo hilo ambalo lilikuwa msitu mkubwa.

Maafisa wa polisi eneo hilo wameishi wakivumilia mvua, kibaridi kikali na kung’atwa na mbu, jambo ambalo baadhi yao waliishia kukosa matumaini na motisha wa kutekeleza majukumu yao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Nyumba, Paul Maringa (kulia) wakati alipozuru Kililana kufungua kituo cha polisi na nyumba za polisi. Picha/ Kalume Kazungu

Aidha ujenzi wa LAPSSET ambao unaendelea eneo hilo sasa umeyapa maisha ya polisi wanaohudumia eneo hilo taswira mpya.

Hivi majuzi kituo kipya cha polisi pamoja na makao mapya ya maafisa hao vilifunguliwa rasmi.

Jengo hilo la kituo cha polisi pamoja na makazi mapya ya maafisa hao viligharimu serikali ya kitaifa kima cha Sh 1.2 bilioni.

Tayari mahema yaliyokuwa yakitumika kama makazi ya polisi yameondolewa  na maafisa wa polisi kuhamia kwenye kituo hicho kipya ambacho kimejengwa kwa muundo wa kisasa na kurembeka, hivyo kukifanya kuwa miongoni mwa vituo bora vinavyovutia kwa macho zaidi nchini.

Tofauti na vituo vingine vya polisi nchini, kituo cha polisi cha LAPSSET pia kiko na zahanati yake mpya ambayo itatumika kuwatibu maafisa wa usalama wanaohudumu eneo hilo.

Zahanati mpya ya polisi iliyojengwa eneo la Kililana. Picha/ Kalume Kazungu

Hali hiyo imepelekea maafisa wengi wa polisi wanaohudumu kaunti ya Lamu kuwa na ari ya kufanya kazi na kuishi eneo hilo la LAPSSET kutokana na makazi na maandhari bora ya maafisa hao kuishi.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, aliisifu serikali kwa kuendeleza mradi wa LAPSSET eneo la Kililana, alioutaja kubadili kabisa hali ya maisha kwa maafisa wake.

Bw Kioi alisema kufunguliwa kwa kituo hicho kipya cha polisi na makazi yao eneo la LAPSSET ni mwamko mpya utakaosaidia kuwapa moyo maafisa wa usalama na kuwafanya kutia bidii zaidi katika kutekeleza majukumu yao.

“Tunafurahia. Ujenzi unaoendelea wa mradi wa LAPSSET eneo hili la Kililana pia umesaidia kubadili maisha ya maafisa wetu. Kwa sasa maisha yameboreka hata zaidi. Maafisa wetu walikuwa wakiishi kwenye mahema lakini kwa sasa wamepata nyumba mpya za kisasa na kituo rasmi cha polisi ambacho pia kina sehemu ya kuwazuilia wahalifu. Hatua hii tayari imewapa motisha maafisa wetu kutia bidiii zaidi kazini,” akasema Bw Kioi.

Mahema ya polisi eneo la Kililana. Picha/ Kalume Kazungu

Kufikia sasa takriba maafisa 100 wa polisi wanahudumia kituo hicho lakini kwa mujibu wa Bw Kioi, zaidi ya maafisa 400 wa vitengo mbalimbali vya usalama wanatarajiwa kusambazwa kituoni humo ili kudhibiti usalama wa bandari ya Lamu punde itakapoanza rasmi shughuli zake.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, ambaye pia ni afisa msimamizi wa Operesheni inayoendelea ya kuwasaka magaidi wa Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni, alitaja kufunguliwa kwa kituo cha polisi cha LAPSSET, makazi mapya na zahanati ya polisi eneo hilo la Kililana kuwa hatua njema itakayowezesha usalama kudhibitiwa zaidi kote Lamu.

“Zahanati iliyoko hapa Kililana ni msaada mkubwa kwa maafisa wetu wa usalama wanaoendeleza operesheni kwenye msitu wa Boni kwani wataweza kuhudumiwa hapa pia. Pongezi kwa serikali yetu. Tutajitahidi kuweka usalama eneo hili ili miradi yote mikuu inayonuiwa kutekelezwa na serikali ifaulu,” akasema Bw Kanyiri.

Kufikia sasa ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza vya LAPSSET umefikia zaidi ya asilimia 60 kukamilika, ambapo kiegesho cha kwanza cha mradi huo kinatarajiwa kukamilika kufikia Juni mwaka huu.

Viegesho vingine viwili vimepangwa kukamilika kufikia mwaka 2020.

Jumla ya Sh 48 bilioni zimekadiriwa kutumiwa na serikali ya kitaifa katika ujenzi wa viegesho hivyo vitatu vya kwanza vya LAPSSET pekee.

You can share this post!

LAMU: Washinikiza mafunzo ya mihadarati yajumuishwe kwa...

Watoto 20 wazaliwa Nakuru mkesha wa Mwaka Mpya

adminleo