• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wanahabari walioshtakiwa kwa mauaji 2018

Wanahabari walioshtakiwa kwa mauaji 2018

Na RICHARD MUNGUTI

WANAHABARI Jacque Maribe na Moses Dola Otieno ni miongoni mwa watu walioshtakiwa kwa mauaji 2018.

Bi Maribe ambaye ni mtangazaji wa runinga alishtakiwa pamoja na mpenziwe Joseph Irungu almaarufu Jowie kwa kumuua mwanamke aliyekuwa akifanya biasha nchini Sudan Kusini Monicah Kimani.

Wapenzi hawa walifikishwa mbele ya Majaji Jessie Lesiit na James Wakiaga kuhusiana na mauaji hayo.

Walikana mbele ya jaji Lesiit ambaye aliamuru kesi hiyo isikizwe na Jaji Wakiaga.

Mbele ya Jaji Kiaga wapenzi hao waliomba waachiliwe kwa dhamana.

Maribe aliachiliwa lakini Jowie akanyimwa dhamana akisemekana kuwa “mla wanawake” kwa vile maisha yake yote amekuwa akiishi na wanawake alio na urafiki nao.

Sasa anaendelea kuzuiliwa katika gereza la Kamiti baada ya kunyimwa dhamana na Jaji Wakiaga aliyesema ni hatari kwa usalama wa mashahidi.

Jowi aliyekuwa amewasilisha ombi Jaji Wakiaga akome kusikiza kesi dhidi yake alipiga abautani na kuondoa ombi hilo ndipo akaruhusiwa kupelekwa hospitali kutibiwa mkono ulio na jeraha la risasi.

Kesi imeorodheshwa kusikizwa mwaka ujao.

Naye Dola aliyeshtakiwa kumuua mkewe aliyekuwa ripota na mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha NTV Sarah Wambui Kabiru miaka saba iliyopita alisukumwa jela miaka 10 na Jaji Roselyn Korir

Punde tu baada ya kuhukumiwa, Dola alisema , “Ni sawa tu. Nitaanza kutumikia kifungo. Nitawasiliana na wakili wangu kuona ikiwa atawasilisha rufaa au la.”

Wakati wa kusomwa kwa hukumu hiyo , watu wa familia ya Wamboi hawakufika kortini.

Wazazi na nduguze Wamboi walipohojiwa na afisa wa urekebishaji tabia walisema, “Kifo cha Wambui kilituuma sana. Tutaishi na kovu la kuuawa kwake milele. Hatujamsamehe mshtakiwa.”

Familia hiyo iliomba korti itekeleze sheria jinsi ilivyo ikimwadhibu mkwe wao.

Jaji Korir alisema taarifa ya familia ya mhasiriwa imeonyesha bado inaumwa na kuuawa kwa binti yao na kusema “adhabu nzuri ni kifungo cha gerezani.”

Dola alisukumiwa kifungo hicho na Jaji Roselyn Korir aliyempata na hatia ya kuua bila kukusudia miaka saba iliyopita katika mtaa wa Umoja mnamo Mei 1, 2011.

Baada ya kumuua mkewe , Dola , alijisalamisha kwa polisi katika kituo cha polisi cha Naivasha kisha akarudishwa kituo cha Buruburu.

Akipitisha hukumu , Jaji Korir , alisema Dola alimuua mkewe kwa sababu ya matatizo aliyokuwa ameyapata kwa kupoteza kazi.

Akauliza Jaji Korir: “Endapo kila mtu aliyepoteza kazi atakuwa akiua mkewe ama mpenziwe ni vifo vigapi vitatekelezwa humu nchini ikitiliwa maanani idadi kubwa ya watu waliopoteza kazi.”

Jaji huyo alisema lazima kila mmoja ajifunze kuvumilia pasi kuchukua sheria mikononi.

“Hii korti itakuwa ainakosea kutomwadhibu mshtakiwa kwa kosa la kumwangamiza  mkewe bila sababu,” alisema Jaji Korir.

Alisema ijapokuwa Dola hakukusudia kumuua mkewe , aliyakatiza maisha ya mkewe ambaye watu wa familia yake walikuwa na matumaini makubwa naye.

Kufikia kifo cha Wamboi alikuwa ripota na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha NTV.

Jaji Korir alisema mshtakiwa aliomba asihukumiwe kifungo cha gerezani mbali afungwe nje kusudi amlee mwanaye.

Wakili Cliff Ombeta aliyemwakilisha Dola aliomba mahakama impe mashtakiwa fursa ya kujirekebisha na kurejeana na wakwe zake.

Jaji Korir alisema kesi dhidi ya Dola ni mojawapo ya kesi ambapo familia na mshtakiwa na familia ya marehemu ziliomba zipewe nafasi ziridhiane.

“Tangu mshtakiwa apatikane na hatia ya kuua familia yake hakuchukua hatua ya kufanya mashauri ya maridhiano. Itakuwa ni ukiukaji wa sheria kutomwadhibu Dola,” alisema Jaji Korir.

Jaji huyo alisema lazima sheria ifuate mkondo na kumwadhibu mshtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Jaji alisema ijapokuwa Bw Ombeta na Dola mwenyewe waliomba korti iwe na huruma ikipitisha hukumu ukweli uliopo ni kwamba mwanaye  Dola “ atakosa mapenzi ya mama kutokana na kitendo cha hasira cha mshtakiwa.”

Akasema Jaji Korir, “Maisha ya Wambui yalikatizwa na mwanawe kupokonywa mapenzi ya mama. Kitendo cha mshtakiwa kilisababisha haya na lazima aadhhibiwe kwa mujibu wa sheria.”

You can share this post!

Watoto 20 wazaliwa Nakuru mkesha wa Mwaka Mpya

Raila awatema washauri wenye misimamo mikali ili kujisuka...

adminleo