• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Wazazi wawinda mkuu wa shule iliyopata ‘E’ nyingi

Wazazi wawinda mkuu wa shule iliyopata ‘E’ nyingi

Na JADSON GICHANA

WAZAZI na wakazi wa eneo la Etago, Kaunti ya Kisii waliandamana jana katika juhudi za kutaka kumng’oa mkuu wa shule ya upili ya Muma baada ya wengi wa watahiniwa kupata alama ya E katika mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) ambao matokeo yalitangazwa mwezi uliopita.

Walidai kuwa mwalimu huyo Bw Lumumba Nyasimi amekuwa mwalimu mkuu kwa miaka kumi na minne katika shule hiyo na kusababisha matokeo mabaya ya mtihani wa KCSE.

Katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa KCSE mtahiniwa aliyeongoza alipata C- huku waliofuatia watano walipata D+, D(16), D-(67) , E(27) na (Y)1.

“Tuliombwa tulipe shillingi 2,000 ya kununua basi la shule miaka mitatu iliyopita na tangu wakati huo hatujaona chochote,”alisema Bw Samweli Okari mzazi katika shule hiyo.

Mwaka wa 2017 matokeo yalikuwa ifuatavyo: B-(1), C+(2), D+(5) na E(28).

Wazazi hao ambao walikuwa na hasira walitishia kuwaondoa watoto wao shuleno hadi usimamizi wa shule hiyo ubadilishwe.

Moses Nyabuto ambaye ni mwenyekiti wa wazazi wa kidato cha pili alisema kuwa walishangazwa sana na hatua ya mwalimu mkuu kutotilia maanani nidhamu ya wanafunzi na kuajiri walimu wa bodi bila kuwajulisha wazazi na pia kuajiri mtoto wake ambaye yuko mwaka wa pili katika chuo kikuu.

Alisema kuwa tangu mwalimu huyo achukue hatamu za uongozi katika shule hiyo ni wanafunzi 12 ambao wamehitimu kuenda chuo kikuu.

Taifa Leo ilipotembelea shule hiyo hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyefika shuleni na ni walimu wachache tu walionekana.

“Sina la kuongea kwa sasa na tafadhali msiniulize swali lolote.Naomba muulize mkurugenzi wa elimu katika Kaunti,” alisema Mwalimu huyo mkuu.

Pia wazazi hao walilalamikia mwalimu huyo kwa kukosa kuwaita wazazi kwa mkutano wa kila mwaka.

“Hatujawahi kuitwa kwenye mkutano wa kila mwaka katika shule tunashuku kwamba kuna kitu mwalimu ametuficha,”akasema Drusila Kwamboka mzazi.

Majengo katika shule hiyo yalikuwa mabovu yaliyojengwa takribani miaka arobaini iyopita na hayajawai karabatiwa takia mwaka wa 1975.

Shule hiyo ambayo iko na wanafunzi Zaidi ya 500 inakosa vifaa muhimu vya masomo vikiwemo miundo msingi .

Aidha, waliandamana hadi ofisi ya Naibu Kamishna katika Kaunti Ndogo ya Etago kuchukua malalamishi yao lakini hawakumpata.

Juhudi za kumfikia mkurugenzi huyo azikufua dafu kwa vile simu yake haiukuwa inachukuliwa.

Walieleza kuwa tayari walituma barua katika ofisi ya elimu katika Kaunti mwezi wa Novemba mwaka uliopita lakini hawajawahi kupata majibu.

Mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti hiyo Dr William Sugut alisema kuwa walipokea malalamishi hayo na jambo hilo linashughulikiwa huku maafisa kadhaa wa elimu wakitumwa katika eneo hilo kufanya uchunguzi zaidi.

“Kama wizara tulipata malalamishi hayo kutoka kwa wazazi na tunashughulikia kwa dharura na tumewatuma maafisa kadhaa sehemu hiyo kufanya uchunguzi zaidi,”akasema.

You can share this post!

Waititu amtuma nduguye Moses Kuria likizo ya lazima zogo...

MUAFAKA: Uhuru aliposhangiliwa na wabunge wa upinzani 2018

adminleo