• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UKATILI: Mama asakwa kwa mauaji ya wanawe watatu

UKATILI: Mama asakwa kwa mauaji ya wanawe watatu

DENNIS LUBANGA na EDITH CHEPNGENO

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Bungoma wanamsaka mwanamke mmoja anayeshukiwa kuwaua watoto watatu kwa kuwateketeza ndani ya nyumba yake kabla ya kutoweka.

Kisa hicho kilitendeka katika kijiji cha Banantega katika eneobunge la Mlima Elgon mnamo Jumatano usiku.

Mama huyo ni mzazi wa wawili kati ya watoto hao wenye umri wa miaka mitano na miwili hali mtoto wa tatu mwenye umri wa miaka mitano ni wa mke mwenza aliyetoweka baada ya kukosana na mumewe miaka ya nyuma.

Mwanamke huyo, ambaye jina lake halikutambuliwa, alipatikana na majirani katika mkahawa mmoja alikojificha baada ya kutekeleza kitendo hicho cha kinyama lakini akaponyoka na kutoroka.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi katika Kaunti ya Bungoma Francis Sang alisema wanamsaka mshukiwa huku wakiendelea na uchunguzi.

“Tunamsaka mwanamke huyo huku tukichunguza tukio hilo kwa lengo la kubaini kulichotokea. Ningependa kutoa hakikisho kuwa tutamkamata mshukiwa,” Bw Sang akasema.

Kulingana na majirani moto ulitokea katika nyumba hiyo mwendo wa saa tatu za usiku watoto hao walipokuwa usingizini.

Lakini juhudi zao za kuwaokoa ziligonga mwamba kwa sababu mlango ulikuwa umefungwa kwa kufuli kutoka nje. Ilibidi majirani kuvunja mlango huo na kuingia ndani.

Majirani pia wanashuku kuwa huenda mumewe mwanamke huyo pia alihusika katika kitendo hicho cha kinyama kwa sababu aligombana na mama wa watoto hao siku mbili kabla ya kisa hicho.

Inasemekana kuwa wazazi hao wawili ni wanywaji pombe wa kupindukia na husababisha vita kati yao kila mara.

“Nilipofika katika eneo la tukio, watoto wawili tayari walikuwa wamechomeka kiasi cha kutoweza kutambulika. Majirani walikuwa wamemkimbiza mwingine hospitalini kabla ya kufariki kutokana na majeraha ya moto,” akasema Mzee Victor Chenanya ambaye ni babu wa marehemu.

Wakati huo huo, watu saba jana walishtakiwa katika mahakama ya Eldoret kwa kushiriki visa vya ubakaji msimu wa krismasi na mwaka mpya.

Saba hao walishtakiwa kwa kuwabaka watoto kati ya umri wa miaka mitatu hadi 16. Wa kwanza kushtakiwa kwa ubakaji ni Andrew Nyongesa, 58 ambaye alikabiliwa na mashtaka mawili.

Bw Nyongesa alidaiwa kumdhulumu kingono mtoto wa miaka mitatu siku ya Krismasi katika kijiji cha Sango, Kaunti ndogo ya Likuyani.

Katika shtaka la pili, Bw Nyongesa alidaiwa kuendeleza kitendo hicho dhidi ya mtoto huyo kwa kumpapasa na kumgusa kwenye sehemu zake nyeti.

Hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Harrison Barasa na akaachiliwa kwa bondi ya Sh200,000 huku kesi hiyo ikiratibiwa kutajwa Januari 21.

Wengine walioshtakiwa kwa makosa ya ubakaji ni Gilbert Wasike, Emmanuel Wekesa, Nathan Kimng’etich, Joseph Simiyu, Duncan Wasike na Ambrose Amunga.

You can share this post!

Wakenya wamkaanga mamaye msichana mlevi mitandaoni

Gavana Nanok kuwaadhibu wafanyakazi wazembe wanaokwama...

adminleo