• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
UVUMBUZI: Teknolojia zitakazovuma 2019

UVUMBUZI: Teknolojia zitakazovuma 2019

NA FAUSTINE NGILA

HUKU teknolojia mpya zikizidi kubuniwa, uvumbuzi duniani na utumizi wa teknolojia zilizopo unabadilisha utendakazi wa kampuni nyingi na jinsi wanadamu wanatangamana.

Maendeleo katika uwezo wa kompyuta kufanya kazi za wanadamu, uchanganuzi wa data kubwa na upanuzi wa mtandao wa intaneti ni mambo yanayochochea mapinduzi haya. Hapa naorodhesha teknolojia kuu zitakazobadilisha maisha mwaka huu.

1. Utumizi wa mashine kufanya kazi za wanadamu

Teknolojia ya roboti inatarajiwa mwaka huu kuwa na sifa kamili za mwanadamu kama kuzungumza, kusoma, kuona, kufikiria na kutambua vitu au watu wanaotembea.

Kwa kutumia teknolojia ya hesabu ya mashine (algorithms) inayowiana na mahali, mashine zitaweza kufanya kazi ambayo inachosha au hatari kwa binadamu, kwa kasi zaidi na kwa umakini zaidi.

Teknolojia hii inatarajiwa kuvuruga kila sekta ya uchumi, huku kampuni nyingi zikiipendelea kwa uwezo wake wa kupunguza gharama na kuongeza ubora.

Mifumo inayohusisha video za 3D, sauti, uwezo wa kushika, kuonyesha maeneo na hata uwezo wa kunusia itabadilisha utendakazi wa mitambo kwa uwezo wake wa kutambua mazingira kwa mbashara.

2. Teknolojia ya Blockchain

Thamani ya sarafu ya dijitali ya Bitcoin imewasisimua watu wengi kutokana na utumizi wake wa teknlojia ya Blockchain.

Hii ni teknolojia salama ya kurekodi na kuthibitisha ununuzi na uuzaji pamoja na uhifadhi wa data muhimu.

Ina uwezo wa kuzima matukio mengi ya kifisadi kama wizi wa pesa kidijitali kwa benki, wizi wa data, wizi wa kura na kutathmini utendakazi wa wafanyakazi huku historia ya watumizi wote wa data ikionekana na kila mtumizi.

Tayari kampuni nyingi duniani zinatumia teknolojia hii, lakini mwaka huu wadau wa teknolojia wanatarajia Blockchain kuanza kutumika kikamilifu hata na serikali na serikali na mashirika.

3. Magari ya kielektroniki

Kuna uwezekano mkubwa mno kuwa kufikia mwishoni mwa 2019, kila kampuni ya kuunda au kuuza magari itakuwa na magari ya kielektroniki kwenye maegesho yake ya mauzo.

Tayari kampuni ya Amerika ya Tesla inauza magari haya ambayo badala ya kutumia dizeli au petroli, yanatumia betri moja hutiwa kwa umeme wakati nguvu zake zimeisha.

Hii inawiana na ajenda ya kimataifa ya kutumia kawi safi, na kukoma kutumia nishati inayotoa moshi.

Magari machache ya kielektroniki tayari yako humu nchini lakini mwaka ukizidi kukomaa tunatarajia idadi yake kuongezeka.

Pia teknolojia ya magari yanayojiendesha yenyewe bila dereva mwanadamu yanatarajiw akutua humu nchini mwaka huu.

4. Malipo ya kidijitali

Tayari tumeshuhusia humu nchini malipo mengi yakifanywa kupitia M-Pesa na Airtel Money, lakini huduma muhimu kama usafiri na ununuzi wa bidhaa umesalia kufanywa kwa sarafu na noti.

Huduma ya kulipia ugeshaji wa magari katika Kaunti ya Nairobi ya eJijiPay na ile ya kutuma na kupokea hela kutoka benki tofauti ya Kenswitch zimeongoza katika malipo ya kidijitali.

Hata hivyo, baadhi ya kampuni nchini Uswidi zimewaweka wafanyakazi wake kidude mkononi ambacho kinatumika kulipia kila huduma na bidhaa.

Kampuni ya Google ina huduma kwa wateja inayoitwa Google Pay huku Apple Inc ikiwa na Apple Pay. Huduma hizi zinatarajiwa kuvumisha malipo ya kidijitali kupitia kwa simu.

Hivyo, hapa Kenya mwaka huu utaona mapinduzi makuu ya malipo ya kidijitali na upungufu wa hela za mkononi kwa kuwa zinawavutia wezi.

5. Uchapishaji wa 3D

Teknolojia hii tayari ni maarufu katika mtaa wa Westlands, Nairobi lakini haijaenea sana katika miji mingine kwa kuwa Wakenya bado hawajatambua uwezo wake.

Ni uvumbuzi unaokuwezesha kutengeneza vifaa vingi vya miundo ainati kama vyombo vya jikoni, samani ya plastiki na vioo.

Lakini katika mataifa yaliyoimarika kiuchumi, teknolojia hii hutumika kujenga nyumba, kutengeneza viungo vya mwili katika matibabu huku pia ikiwa na uwezo wa kupika vyakula kama pizza.

Mtumizi hutakiwa kuchora muundo wa chombo anachotaka kutengeneza kwa kutumia kompyuta kwanza. Kisha mashine ya uundaji hujazwa na viambato vya kutengeneza chombo hicho kama plastiki iliyosagwa kuwa uji kisha kubonyeza kitufe cha ‘Chapisha’.

Ikiwa teknolojia hii inatumika mijini, utaanza kuona uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka mataifa ya nje ukipungua.

6. Uzinduzi wa mtandao wa 5G

Kizazi cha tano cha teknolojia isiyotumia waya inatazamiwa kutawala matumizi ya simu kote duniani.

Hii ndiyo teknolojia itakayochukua nafasi ya Wi-Fi, kwani itapunguza muda wa kutuma na kupokea data kwa intaneti kutoka milisekunde 30 hadi milisekunde moja pekee.

Hii itaongezea uzito wa muunganisho baina ya mashine mbili kwenye mtandao.

Tofauti na Wi-Fi ambapo data inaweza kuzuia na kutekwa, 5G data itakuwa salama huku mtandao wa kibinafsi wa 5G ukiwezesha upakiaji na upakuaji wa data kubwa.

Kasi ya intaneti itakuwa juu zaidi, na kutazama video ndefu au kuipakia kwa YouTube kutakuwa haraka zaidi, ukitumia kompyuta, tableti au simu.

You can share this post!

EPL: Breki kwa Liverpool Etihad

Uhuru apondwa ngome yake

adminleo