• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Uhuru apondwa ngome yake

Uhuru apondwa ngome yake

FRANCIS MUREITHI, STEVE NJUGUNA Na GRACE GITAU

VIONGOZI zaidi kutoka eneo la Mlima Kenya wamejitokeza kumkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa madai ya kupuuza eneo hilo kimaendeleo.

Hapo Jumapili, Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri (pichani) aliungana na mwenzake wa Gatundu Kusini, Moses Kuria kudai Serikali ya Jubilee haijawafaa wakazi wa Kati kimaendeleo licha ya kuiunga mkono kwa dhati kwenye chaguzi za 2013 na 2017.

Wabunge Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati) na Gichuki Mugambi (Othaya) pia walimuunga mkono Bw Kuria wakisema ni haki yake kudai maendeleo kutoka kwa serikali.

Bw Mugambi alisema kila kiongozi ana haki ya kutetea watu wake: “Nani atazungumzia matatizo yanayowakabili wapigakura ikiwa sio viongozi? Hakuna anayefaa kuzuiwa kutoa maoni yake.”

Lakini ni Bw Ngunjiri aliyechemkia Rais Kenyatta zaidi akisema wakazi wa Mlima Kenya wameteseka zaidi chini ya utawala wake na kama ameshindwa kuongoza aitishe uchaguzi.

“Watu katika sekta ya jua kali Nairobi, wauzaji mbao Nakuru na maeneo mengine ya Rift Valley wanalia. Hii Serikali haijasaidia jamii ya Mlima Kenya kiuchumi na kisiasa kujiendeleza. Wakazi wamo katika hali mbaya zaidi chini ya utawala wa Rais Kenyatta,” alisema Bw Ngunjiri.

Akionekana mwenye machungu, Bw Ngunjiri alisema Rais Kenyatta anafaa kujitenga na Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe kwa matamshi yake dhidi ya Naibu Rais William Ruto kuhusu urithi wa urais 2022.

“Jubilee si chama cha mtu mmoja. Rais iwapo utaacha watu kama Murathe kuendelea kutoa matamshi ya kugawanya Wakenya utaacha Kenya ikiwa imegawanyika zaidi. Iwapo Rais Kenyatta amechoka kuongoza nchi anafaa kuitisha uchaguzi mara moja ili tumalize uvumi uliopo wa kisiasa,” akaeleza.

Alimtetea Bw Ruto akisema ndiye aliyeongoza kampeni za Rais Kenyatta na kama sio uungwaji wake hangeshinda, na kwa kukataa kumuunga mkono 2022, jamii ya Mlima Kenya itaonekana kuwa ya watu waongo kisiasa.

Naye Bw Kuria alirejelea matamshi yake akisema eneo la Mlima Kenya halijapata matunda ya utawala wa Jubilee licha ya kuiunga mkono kwa wingi.

“Serikali ya Jubilee haijatimiza ahadi zake kwa eneo la Mlima Kenya. Maeneo mengi yamebaki nyuma kimaendeleo. Barabara ni mbaya, stima hakuna, maji hakuna… licha yao kuendelea kuunga mkono Serikali,” akasema akiwa eneo la Ol Kalou wakati wa mazishi ya afisa mkuu wa kwanza wa benki ya Equity, Mwangi Kagema mnamo Jumamosi.

Alieleza haja ya kubadili mfumo wa ugawaji raslimali kwa kaunti akisema mfumo wa sasa unanyanyasa sehemu zilizo na idadi kubwa ya watu kama vile Mlima Kenya.

Bw Kuria alisema kaunti nyingi za eneo la Mlima Kenya zinachukuliwa kama zilizoendelea na hivyo zinagawiwa pesa chache.

“Hii ndiyo sababu tunapaswa kubadilisha mfumo huu baada ya sensa ili rasilmali ziweze kugawa kwa usawa. Watu hawafai kuteseka tena.”

Bw Kuria alisikitika kuwa kwa sababu ya mfumo wa sasa wa kugawa mapato ya serikali, wakazi wa eneo la Mlima Kenya wameendelea kuteseka katika umasikini.

You can share this post!

UVUMBUZI: Teknolojia zitakazovuma 2019

Uamuzi wa Jumwa na Dori kutimuliwa ODM wakaribia

adminleo