• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
OBARA: Kampeni za mapema za urais zimefungua macho wananchi

OBARA: Kampeni za mapema za urais zimefungua macho wananchi

Na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wengi wa kisiasa wamelaumiwa kwa kuanzisha kampeni za mapema za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika 2022 ilhali utawala wa rais wa sasa haujakamilisha miaka miwili mamlakani.

Wanasiasa hao wamelazimika kutumia muda na raslimali nyingi kwa kampeni hizo badala ya kuzitumia kuimarisha maendeleo yatakayonufaisha wananchi wa kawaida.

Lakini kuna jambo jema kuhusu joto hili la kisiasa. Kwa mara ya kwanza, wapiga kura wamepata fursa ya mapema kujionea aina ya viongozi ambao hawana ari yoyote ya kuwatumikia. Kwa sasa, suala ambalo linazidi kuibua mjadala mkali katika siasa za Kenya ni mustakabali wa Naibu Rais William Ruto katika Chama cha Jubilee.

Hii ni baada ya Naibu Mwenyekiti wa chama hicho, Bw David Murathe, kudai jamii ya Agikuyu haina deni lolote la kisiasa kwa Bw Ruto, huku naye Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju akisema ni lazima naibu rais apitie mchujo endapo ataazimia kupeperusha bendera ya Jubilee uchaguzini.

Kama ilivyotarajiwa, matamshi ya wawili hao yaliibua mtafaruku wa kisiasa Jubilee na kuzidisha msisimko wa kisiasa kitaifa.

Kuna jambo aliloangazia Bw Murathe ambalo ni mfano mwema wa baraka wapigakura wanastahil kufurahia kutokana na kampeni za mapema.

Kwenye hotuba yake katika Kaunti ya Vihiga, Bw Murathe hakuficha kwamba wanataka mgombeaji urais atakayejali masilahi ya jamii yake.

Kwa miaka mingi, Wakenya wamekuwa wakiambiwa wajihadhari na aina ya viongozi wanaowania viti mbalimbali vya kisiasa kwa kuwa wengine wao hunuia tu kulinda masilahi yao ya kibinafsi, ya familia zao na wandani wao wa karibu.

Bila shaka, si kawaida kusikia mwanasiasa akikiri hadharani kwamba ana masilahi ya kijamii ambayo yanamsukuma kuamua kiongozi anayestahili kuchaguliwa kuongoza taifa.

Wadhifa wa urais una jukumu kubwa la kuongoza nchi hii lakini umekuwa ukidunishwa tangu Kenya ilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Tumepitia enzi ambapo watu wachache walijitolea kulinda utawala wa kiimla ili wapate nafasi za kupora rasilimali za umma. Sasa tumefikia enzi ambapo makundi ya watu yanatetea utawala usiojali mwananchi wa kawaida ili wao na wandani wao wapate zabuni serikalini.

Zabuni hizo ndizo zimekuwa zikitumiwa kufuja mali ya umma katika miaka ya hivi majuzi hadi Rais Uhuru Kenyatta alipokumbuka kuhusu sifa anazotaka kuacha atakapokamilisha hatamu yake ya pili na ya mwisho uongozini.

Ingawa Bw Murathe hakufafanua wazi kuhusu masilahi ambayo angetaka rais ajaye alinde kwake na jamii yake, ninachoweza kubashiri ni kuwa, mengi hayahusu mkulima mdogo katika eneo la Kati au Mlima Kenya anayejikakamua kutafutia familia yake riziki huku akilemewa na mzigo mkubwa wa ushuru.

Kwa kuwa tumeshindwa kuzuia kampeni za mapema, ni vyema tuwafahamu wanasiasa hawa na nia zao mapema kabla tufike uchaguzini.

Tujue kuwa matatizo yanayotukumba hayatatatuliwa na rais aliye ‘mfalme wa kijamii’ bali kiongozi aliyedhihirisha uzalendo na uaminifu kwa taifa lote.

You can share this post!

Wakazi wakataa kupanga uzazi, wasema idadi yao itapungua

TAHARIRI: Waziri wa Elimu awe na msimamo rasmi

adminleo