• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wanawake Saudia kutalikiwa kupitia SMS

Wanawake Saudia kutalikiwa kupitia SMS

MASHIRIKA na PETER MBURU

MAHAKAMA nchini Saudi Arabia zimetangaza kuwa wanawake wa nchi hiyo wataanza kufahamishwa na mabwana zao kuhusu talaka kupitia ujumbe mfupi kwa njia ya simu.

Hatua hiyo inalenga kumaliza visa vya wanaume nchini humo kuwataliki wake zao bila kuwajulisha, zikasema mahakama.

Kuanzia Jumapili, korti zilianza kile zilizoita “hatua inayolenga kulinda haki za wateja wa kike, na kuhimiza mabadiliko ya kidijitali kwa huduma zaidi,” wizara ya haki Saudi ikasema kupitia habari.

Ujumbe wa simu atakaotumiwa mwanamke utahusisha nambari ya cheti cha talaka na jina la korti iliyoamrisha talaka yenyewe ambapo anaweza kupokea nakala zake akitaka.

Wanawake aidha wataweza kufahamu kuhusu hali zao za ndoa kupitia tovuti na kufahamu kuhusu ikiwa kumekuwa na kuharamishwa kwa vyeti vyao vya ndoa.

Hatua hiyo ya serikali imekuja wakati mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayoitwa Vision 2030 ambayo yanasukumwa na mtawala wa taifa hilo Mohammed bin Salman yameshika kasi. Mabadiliko hayo yanahusisha wanawake kuruhusiwa kuendesha magari.

Bin Salman ni mtawala aliyekuwa amejipa sifa ya mtu wa mageuzi, kabla ya kisa cha Oktoba mwaka uliopita ambapo mwanahabari Jamal Khashoggi aliuawa kinyama katika ubalozi wa Saudi nchini Uturuki, huko Instanbul.

Serikali ya Saudi hata hivyo ilikana kuwa bin Salman alihusika katika mauaji hayo.

You can share this post!

Ingwe motoni baada ya mashabiki kumpiga refa

Juhudi za wanajeshi kupindua serikali Gabon zaambulia pakavu

adminleo