• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Matiang’i anaweza kumrithi Uhuru 2022 – Arama

Matiang’i anaweza kumrithi Uhuru 2022 – Arama

FRANCIS MUREITHI na PETER MBURU

MBUNGE wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama amedai kuwa waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ameiva vya kutosha kuiongoza Kenya kama Rais, akisema kuwa urais humu nchini sio wa baadhi ya jamii tu.

Bw Arama alidai kuwa utendakazi wa Dkt Matiangi umedhihirisha kuwa yeye ni afisa anayeweza kuwafanyia Wakenya maendeleo, hivyo akisema kuwa pia naye anaweza kumridhi Rais Uhuru Kenyatta baada yake kustaafu 2022.

Alisema katika uchaguzi ujao, atampigia debe waziri huyo kuwania urais, kwa kurai jamii yake kumuunga mkono.

“Tuna watu kama Dkt Fred Matiangi ambaye amedhihirisha kuwa ana uwezo wa kuwa Rais atakayefuata wa Kenya na nitasukuma jamii yangu kumfikisha debeni kwani sharti tuonyeshe jamii nyingine kuwa kiti hicho si cha jamii teule,” akasema Bw Arama.

Bw Arama alikuwa akizungumza Jumatatu katika ofisi ya CDF eneobunge hilo, ambapo alitoa zaidi ya Sh4.1milioni za basari kwa wanafunzi 200 wa eneo lake.

Mbunge huyo alisema kuwa wazo lililo na jamii tatu kubwa za Kenya kuwa ndizo zinafaa kuongoza taifa hili linafaa kukomeshwa.

“Hizi jamii zinazungumzia sana uchaguzi wa Urais 2022 ni kama jamii zingine, ikiwemo ya Kisii ambayo imetoa waziri chapa kazi zaidi hazina uwezo wa kutoa mgombea Urais,” akasema Bw Arama.

Alidai kuwa baadhi ya viongozi wa jamii Fulani wanasukuma kuwe na mabadiliko ya kikatiba ili Rais Kenyatta atengewe nafasi, ilhali hata hajaeleza nia yake ya kutaka kiti chochote.

You can share this post!

Mafuta ya kubadili rangi ya ngozi yaondolewa madukani Rwanda

Afueni kwa Echesa na Matiang’i korti kuamuru wasilipe...

adminleo