• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Watu wasahaulifu sana wana akili nyingi – Utafiti

Watu wasahaulifu sana wana akili nyingi – Utafiti

MASHIRIKA na PETER MBURU

WANASAYANSI wamebaini kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya mtoto anayesahau mambo wakati mwingi na kiwango cha juu cha werevu, wakisema kuwa uwezo wa kukumbuka mambo si ishara ya werevu.

Wanasayansi hao walisema kuwa katika akili ya mtoto, kusahau ni sehemu kuu katika werevu, kwani kuna maana sawa tu na kukumbuka.

Ripoti ya mtafiti Paul Frankland ambaye hutafiti akili za watoto na namna zinavyofanya kazi ilisema kuwa akili za binadamu husahau kila mara na hivyo hicho si kitu kibaya.

Mtafiti mwingine kutoka chuo kikuu cha Toronto aidha alipata matokeo sawia katika utafiti wake wa kisayansi.

Matokeo yao yalibaini kuwa kusahau ni sehemu kubwa katika akili ya binadamu, sawa na kukumbuka.

Walisema kuwa lengo la akili si kuhifadhi habari zilizo na umuhimu, ila kutumiwa vyema kufanya maamuzi ya busara, kwa kuhifadhi habari zinazohitajika tu.

“Lengo la akili ni kuelekeza hali ya kufanya maamuzi,” chuo kikuu cha Toronto kupitia Profesa Blake Richards kikasema.

“Ni muhimu kuwa akili zisahau habari zisizohitajika na badala yake kushughulika na zile zitasaidia kufanya maamuzi ya umuhimu kwa maisha,” akasema.

Ripoti yao ilisema kuwa mtu anapokumbuka sehemu fulani tu ya mazungumzo ama tukio badala ya kila kitu, inamaanisha kuwa akili zake husahau mambo. Hata hivyo, iliendelea kusema kuwa akili za namna hiyo ni za umuhimu kwa kufanya maamuzi ya kimaisha ama kubashiri siku za usoni.

Kulingana na watafiti hao, sababu ya akili kusahau mambo ni kwa ajili ya kuhifadhi habari zingine ambazo zinakumbana nazo kwani kila siku kuna matukio tofauti.

Aidha, walisema kusahau humsaidia mtu kufanya maamuzi ya busara kwa kutumia matukio ya mbeleni kubashiri mapya yanayokuja.

“Umuhimu wa akili ni kumsaidia mtu kufanya maamuzi yanayofaa anapokumbana na kitu kipya, wala si kukumbuka matukio ya miaka ya zamani. Ili hilo kuwezekana, akili zinafaa kusahau ili ziwe na nafasi ya kutosha,” Bw Richards akasema.

You can share this post!

Mwanaume avamia shule kwa nyundo na kujeruhi watoto 20

Chama cha Jubilee chasimama na ‘Baba’

adminleo