• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Viongozi Nakuru watisha kumng’atua Kimani Ngunjiri

Viongozi Nakuru watisha kumng’atua Kimani Ngunjiri

MACHARIA MWANGI na MAGDALENE WANJA

BAADHI ya viongozi kutoka eneobunge la Bahati wametishia kuanza mchakato wa kumwondoa mamlakani mbunge Kimani Ngunjiri kwa kuongoza maandamano ya kumpinga Rais Uhuru Kenyatta mjini Nakuru.

Viongozi hao waliojumuisha madiwani wa zamani, walisema kwamba mbunge huyo anapaswa kuondolewa uongozini kwa kumkosea heshima Rais Kenyatta. Waliongozwa na mabw Stece Kihara na Njuguna Gichamu.

“Hatuwezi kumruhusu kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kumkosea heshima kiongozi wa nchi kwa kufanya maandamano dhidi yake. Tutaanza mchakato wa kumwondoa mamlakani kwa kukusanya saini,” akasema Bw Kihara.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NGCDF) ya eneo hilo Anthony Njui alisema kwamba ni kinaya kwa Bw Ngunjiri kudai kwamba serikali haijafanya lolote, ilhali hawezi kueleza alivyotumia zaidi ya Sh600 milioni za hazina hiyo kwa miaka mitano iliyopita.

“Bw Ngunjiri amepoteza mwelekeo. Anapaswa kuwaambia wakazi alichofanya kwa Sh600 milioni alizotengewa na Serikali ya Kitaifa,” akasema Bw Njui.

Wakati huo huo, Chama cha Wazee wa Jamii ya Agikuyu (Kiama Kia Ma) kimekashifu vikali matamshi ya Bw Ngunjiri, kwa kuyataja kama “yasiyo hekima.”

Matamshi hayo pia yamekashifiwa na Chama cha Wazee wa Naivasha, kinachojumuisha wazee kutoka jamii mbalimbali zinazoishi katika eneo hilo.

Viongozi hawa wa Nakuru wametishia kumuondoa mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri mamlakani kwa kutomdharau rais. Picha/ Maggy Wanja

Mwenyekiti wa Chama cha Wazee wa Jamii ya Agikuyu katika Kaunti ya Nakuru (NCKCA) Mathew Njoroge ndiye alikuwa wa kwanza kumkashifu mbunge huyo kwa kumdharau rais na wanachama wa chama hicho.

Bw Njoroge alimlaumu Bw Ngunjiri kwa kukosa kuzingatia taratibu za chama hicho katika kuangazia masuala yanayoiathiri jamii.

“Akiwa mwanachama wetu, anafahamu kuhusu taratibu ambazo huwa tunazingatia. Kutoa tamko la kumtukana Rais ni kumkosea heshima na kudunisha nafasi yetu katika jamii,” akasema.

Hata hivyo, hakueleza ikiwa mbunge huyo atachukuliwa hatua za kinidhamu, akisisitiza tu kwamba huwa wana taratibu ambazo hufuatwa katika kuwaadhibu “wanaokiuka” kanuni zake.

Chama hicho kinaheshimika sana katika jamii ya Agikuyu, kwani huwa kinahusika katika utoaji adhabu dhidi ya wanachama ambao wanakiuka taratibu zilizowekwa. Miongoni mwa adhabu kuu ambazo hutolewa ni kuwakabili wale wanaowakosea heshima wale walio uongozini.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Wazee cha Naivasha, Daniel Kariuki, alisema kuwa lazima Bw Ngunjiri aombe msahama kwa Rais Kenyatta.

“Kama wanachama wa baraza la wazee, tunahisi kusikitishwa sana na vitendo vya Bw Ngunjiri ambaye ni mwanasiasa mkongwe,” akasema Bw Kariuki.

Alisema kwamba mbunge huyo alipaswa kuomba ushauri na wanachama wa baraza hilo kabla ka kwenda hadharani kutoa matamshi kama hayo.

Alisema kwamba wazee wanaunga mkono kikamilifu juhudi za Rais Kenyatta kuiunganisha nchi kwa ushirikiano na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga.

“Siasa za 2022 hazipaswi kuanzishwa wakati huu. Rais na Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakisisitiza kwamba lengo lao kuu ni kutekeleza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za serikali yao,” akasema Bw Kariuki.

You can share this post!

Mwanamume asakwa kwa mauaji ya babake

Msongamano wa wanafunzi waathiri elimu ya chekechea

adminleo