• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Wavinya Ndeti amtetea Kalonzo dhidi ya mahasimu

Wavinya Ndeti amtetea Kalonzo dhidi ya mahasimu

Na STEPHEN MUTHINI

ALIYEKUWA mgombeaji wa ugavana katika Kaunti ya Machakos kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, Bi Wavinya Ndeti, amemtetea Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka dhidi ya madai kuwa yeye ndiye alimpelekea kushindwa uchaguzini na Kiongozi wa Chama cha Maendeleo Chap Chap, Dkt Alfred Mutua. Bi Ndeti alisisitiza hakushindwa kwa njia ya haki kama inavyodaiwa na mahasimu wake.

Akizungumza kwenye mazishi katika eneo la Thinu, Kaunti ya Machakos mnamo Jumamosi, Bi Ndeti alisema bado ana imani kwa kiongozi wake wa chama akaongeza inasikitisha jinsi magavana watatu wa eneo la Ukambani wameungana kumpiga vita Bw Musyoka.

“Ninashangaa kuwa magavana watatu wameungana dhidi ya Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka. Wakome kumlaumu kiongozi wetu wa chama kwa ukosefu wa maendeleo katika eneo hilo. Kiongozi wa chama chetu hapewi pesa za maendeleo, wao ndio wana pesa hizo,” akasema Bi Ndeti.

Hisia sawa na hizo zilitolewa na kikundi cha viongozi wa kanisa na wazee ambao walitoa taarifa kwa vyombo vya habari Machakos Alhamisi iliyopita.

Walitetea mafanikio yaliyoletwa na Bw Musyoka katika uongozi wa jamii ya Ukambani na kusema alileta umoja katika jamii na kuiwezesha kupigania nafasi yao serikalini.

Lakini wapinzani wa Bw Musyoka wanasema uwakilishi wa jamii hiyo katika serikali imepungua tangu Bw Musyoka aliposhika usukani kutoka kwa aliyekuwa kigogo wa kisiasa za Ukambani, marehemu Mulu Mutisya.

Wale wanaomtetea walisema wakosoaji wa Bw Musyoka wanaosema hajapeleka maendeleo katika eneo hilo hawazingatii kwamba hajawahi kutumikia kama gavana na wala hasimamii bajeti kubwa kama magavana wanavyofanya.

Wakizungumza katika makao makuu ya Kanisa la African Brotherhood mjini Machakos, kikundi cha viongozi wa jamii ya Wakamba ambacho husimamia Jumuiya ya Kiuchumi Mashariki mwa Kenya (SEKEB) kilisema midahalo ya kisiasa si mibaya lakini wanasiasa wanafaa wajiepushe kutusiana.

Askofu Mkuu Timothy Ndambuki wa kanisa la ABC alisema Bw Musyoka ametimiza mafanikio mengi katika kuleta umoja wa jamii ya Wakamba.

Bw Ndambuki ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa SEKEB alisema si rahisi viongozi wote wa jamii kukubali kuhusu mafanikio yaliyoletwa na kiongozi huyo wa Wiper.

“Bw Musyoka amefanikisha mengi. Wanasiasa wanasema hajakuwa akishauriana nao lakini tunaamini amekuwa akitafuta mwafaka kwa niaba yetu,” akaongeza. Mbali na Dkt Mutua, magavana waliomkosoa Bw Musyoka ni Charity Ngilu (Kitui) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni).

You can share this post!

Serikali kutathmini deni la Sh2b kufichua wanakandarasi hewa

Nyumba 40 zilizojengwa kwa ardhi ya KPA kubomolewa

adminleo