• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Al Shabaab wadai kutekeleza shambulio la 14 Riverside, Westlands

Al Shabaab wadai kutekeleza shambulio la 14 Riverside, Westlands

Na PETER MBURU 

KUNDI la kigaidi kutoka Somalia, Al Shabaab Jumanne limedai kutekeleza shambulizi jijini Nairobi eneo la 14 Riverside, mtaani Westlands.

Kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter, kundi hilo lililohojiwa na shirika la habari la Al Jazeera, lilidai kuwa “kuna operesheni tunayofanya jijini Nairobi.”

Hata hivyo, vikosi mbalimbali vya polisi vilitumwa eneo la Riverside, Westlands, baada ya hoteli ya Dusit kuvamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa magaidi na kulipua na kuanza kupiga risasi.

Watu hao, ambao idadi yao bado haijajulikana wanadaiwa kufika katika hoteli hiyo saa za alasiri, katika kisa ambapo magari yaliyokuwa yameegeshwa eneo hilo yaliteketezwa.

Aidha, makumi ya watu ambao walikuwa ndani ya jingo hilo bado walikuwa wamezuiliwa humo, ndani wengi wao wakihofia maisha.  Vamizi hilo liliwapelekea Wakenya, pamoja na watu waliokuwa ndani ya jingo wakijificha kutumia mitandao ya kijamii kufahamishana na kuhamasishana kuhusu shambulio hilo huku baadhi ya watu waliodai kuwa mateka humo ndani wakiitumia kuitisha msaada.

Vilevile, Wakenya walitumia mitandao kujukumisha asasi za usalama kufika eneo hilo kwa haraka, kwa kuanzisha kampeni katika mtandao wa Twitter, wakitumia majina Riverside, Dusit na Westlands.  Bwana mmoja kwa jina Ron Ng’eno alisambaza jumbe kadha, akieleza namna alikuwa amejificha bafuni, na kueleza namna alivyohofia maisha yake.

“Niko eneo la 14 Riverside drive nimejificha ndani ya bafu na tumevamiwa,” Bw Ng’eno akatuma ujumbe mwendo was aa tisa na dakika 40. “Nikifariki, nampenda Mungu na ninaamini nitaenda mbinguni, tafadhali ambieni familia yangu nawapenda, nakupenda Cleb, Mark na Carol,” akasema dakika nne baadaye.

“Tafadhalini fahamisheni ubalozi wa US humu nchini na idara ya polisi. Niko Riverside drive karibu na dusitd2. Kumetokea mlipuko mkubwa kisha milio ya risasi, sasa nimejificha chooni,” akasema dakika 16 baadaye.

Akaunti ya jamaa huyo ilieleza kuwa yeye ni bwana, baba, mshauri wa mawasiliano na mpiga picha.  Mtumizi mwingine wa twitter kwa jina Kebaya @armchairtycoon alisema “Nimeponea vamizi la kigaidi eneo la Riverside. Mili imetapakaa kila mahali. Mabomu kila mahali.”

Geoffrey Njenga naye alichapisha “14 riverside imevamiwa. Tafadhali tusaidieni tunajificha. Magaidi waliovalia magwanda meusi na waliojihami vikali.”  Maureen Nkirote pia kwenye twitter alidai kuwa alikuwa amejificha ofisini, akisema “tafadhali tuwekeni katika maombi.”

“Tumezuiliwa katika ofisi zetu eneo la 14 riverside, jeongo la hanover. Tuko kama 16. Tafadhali tuokoeni,” akasema Joseph Ndwiga.  Saa kumi na dakika 38, idara ya polisi ilituma ujumbe kwenye twitter, ikidhibitisha kuwa kulikuwa na tukio la uvamizi eneo hilo, na kusema “eneo hilo limezuiwa na kupitwa na wasafiri wanashauriwa kutumia njia mbadala ili kurahisisha kazi ya polisi.”

Idara ya DCI aidha ilirejelea ujumbe huo muda mfupi baadaye.  Baadhi ya watu waliotuma jumbe kueleza kuwa wana watu wanaowajua na ambao walikuwa ndani ya jingo hilo ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

“Rafiki yangu anafanya kazi katika ofisi zilizoko 14 Riverside. Anasema kuna vamizi katika jingo lao. Tafadhali idara ya polisi, mnaweza kulinda eneo hilo?”

Watu wengine walizidi kumimina jumbe kwenye mitandao, wengine wakieleza walipojificha na kuomba msaada wa kuokolewa, huku wengine nao wakieleza kuhusu watu wa familia yao ama marafiki ambao walikuwa humo ndani.

You can share this post!

Mwanaume ahadaa majirani anazika paka, kumbe ni mwanawe!

SHAMBULIO: New York Times yakumbana na ghadhabu za Wakenya...

adminleo