• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Kenya yashuka hadi nafasi ya 106 viwango vya FIFA

Kenya yashuka hadi nafasi ya 106 viwango vya FIFA

Harambee Stars washerekea bao dhidi ya Burundi katika mchuano wa CECAFA 2017. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeteremka nafasi moja kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Alhamisi.

Mabingwa hawa wa Cecafa Senior Challenge Cup mwaka 2017 wanashikilia nafasi ya 106 duniani.

Wako katika nafasi ya 26 barani Afrika kutoka nambari 25 na wanasalia katika nafasi ya pili katika eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Tunisia inasalia nambari moja Afrika na 23 duniani. Inafuatiwa na Senegal (chini nafasi tatu hadi 27 duniani), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (imepaa nafasi nne juu hadi 39 duniani), Morocco (chini nafasi tatu hadi nambari 42 duniani) nayo Misri inafunga mduara wa tano-bora baada ya kuporomoka nafasi 13 hadi nambari 43 duniani.

Cameroon (chini nafasi sita hadi 51 duniani), Nigeria (imeteremka nafasi moja hadi 52 duniani), Ghana (imeshuka nafasi nne hadi 54 duniani), Burkina Faso (imetupwa chini nafasi 13 hadi 57 duniani) na Algeria (chini nafasi tatu hadi nambari 60 duniani) zinashikilia nafasi za sita hadi 10 barani Afrika.

 

Uganda yaongoza Afrika Mashariki

Katika eneo la Cecafa, Uganda inasalia nambari moja katika nafasi ya 78 duniani baada ya kuteremka nafasi tano.

Kenya ni ya pili (106 duniani), Rwanda (juu nafasi mbili hadi 114 duniani), Sudan (imeimarika nafasi sita hadi 118 duniani), Ethiopia (imepaa nafasi mbili hadi 138 duniani), Burundi (imesalia 143 duniani), Tanzania (imekwamilia 146 duniani), Sudan Kusini (haijasonga kutoka nafasi ya 153 duniani) na Djibouti (inasalia nambari 187 duniani). Eritrea na Somalia zinaendelea kuvuta mkia katika nafasi ya 206 duniani.

Hakuna mabadiliko katika nafasi 17 za kwanza duniani ambapo Ujerumani inafuatwa na Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Uhispania, Poland, Uswizi, Ufaransa, Chile, Peru, Denmark, Colombia, Italia, Croatia, Uingereza na Mexico katika usanjari huo. Misri na Burkina Faso ni mataifa yaliyoshuka sana (nafasi 13) nayo Congo Brazzaville iliimarika katika orodha hii ya mataifa 206. Congo inashikilia nafasi ya 88 baada ya kuruka juu nafasi nane.

You can share this post!

Chipukizi 99 kung’ang’ania nafasi katika...

Mawaziri wapya wahimizwa kuzingatia usawa kwenye utendakazi

adminleo