• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Askofu aombwa akatae gari alilopewa na Ruto

Askofu aombwa akatae gari alilopewa na Ruto

Na SIAGO CECE

MWANAHARAKATI mmoja wa haki za binadamu anataka gari aina ya Mitsubishi Pajero ambalo Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kisumu, Philip Anyolo alizawadiwa na Naibu Rais William Ruto, liuzwe na pesa zitakazopatikana zigawiwe masikini.

Padre Gabriel Dolan alisema kama sadaka, zawadi zinazotolewa kwa kanisa hazifai kutolewa hadharani na kutangaziwa umma.

“Asasi za kidini hazifai kupokea michango hadharani kutoka kwa viongozi wa kisiasa waliochaguliwa au walioteuliwa. Zawadi kama hizo zinafaa kuwa za kibinafsi na kutolewa kwa siri kama zile za waumini wengine,” alisema.

Alisema iwapo watu wana chochote cha kupatia kanisa, wanafaa kufanya hivyo kwa siri na akashangaa Naibu Rais alikopata utajiri wake.

“Kanisa halifai kuipokea. Alitoa wapi pesa hizo? Hasa wakati kuna maswali kuhusiana na maadili yake, kanisa linafaa kukataa hadi utajiri wake ujulikane ulitoka wapi, hatufai kupokea zawadi hizi,” alisema.

Padre Dolan alionya kanisa akisema, linafaa kusaidia kupiga vita ufisadi.

“Kanisa linafaa kuwa kwenye msitari wa mbele kupiga vita ufisadi na sio kupokea utajiri ambao hatujui ulitoka wapi. Ni muhimu pia kutenga siasa na kanisa. Ikiwa watakupatia pesa nyingi hivi unawezaje kuwakabili wanasiasa kuhusu masuala ya uadilifu ilhali unapokea zawadi kutoka kwao?” alisema.

Aidha, aliwataka viongozi wa kanisa kuwa na msimamo ikiwa pesa na zawadi nyingine zinapaswa kukubaliwa na iwapo kuna shaka kuhusu anayezitoa, kanisa linafaa kuzipokea au kukataa.

Mwanaharakati huyo alikuwa akizungumza katika mahakama ya watoto ya Tononoka, Kaunti ya Mombasa ambapo shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Yetu, lilitoa masanduku ya kulinda mashahidi.

Alisema shirika hilo lilitoa masanduku hayo ili kusaidia watoto waliodhulumiwa kimapenzi kutoa ushahidi bila kutambuliwa.

“Ikiwa ni kesi ya unajisi, au kesi yoyote inayohusu mtoto ni muhimu kwa mtoto huyo kulindwa wakati wa kutoa ushahidi. Watoto huathiriwa na hawawezi kutoa ushahidi kwa sababu ya kuogopa waliowadhulumu,” alisema Padre Dolan

Hakimu Mkuu Mkazi Viola Yator alisema kesi nyingi huwa zinaahirishwa kwa sababu ya mtoto kuogopa kutoa ushahidi.

“Kwa kutumia masanduku haya, basi watoto hawataogopa kutoa ushahidi,” alisema Bi Yator .

Haki Yetu lilitoa masanduku 10 katika korti za kaunti za pwani zikiwemo za Shanzu, Kilifi, Malindi, Kwale na Mombasa.

Triza Gacheru, wakili wa Haki Yetu, alisema hatua hiyo itahakikisha haki itatendeka

“Kuna kesi nyingi za unajisi katika eneo la Pwani na hii itasaidia ziendeshwe vyema kwa kuhakikisha watoto wanapata haki,” alisema Bi Trizer Gacheru.

You can share this post!

SHAMBULIO: Matukio makuu ya kigaidi awali hapa Kenya

John Baraza kuinoa Sofapaka tena baada ya kocha kujiuzulu

adminleo