• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:55 AM
John Baraza kuinoa Sofapaka tena baada ya kocha kujiuzulu

John Baraza kuinoa Sofapaka tena baada ya kocha kujiuzulu

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mwaka wa 2008 Sofapaka, Melis Medo, Jumanne Januari 15 alijiuzulu wadhifa huo baada ya kusimamia mechi saba pekee za timu hiyo msimu huu.

Kocha huyo aliyeungana na Batoto ba Mungu kutoka klabu ya Nakumatt(kwa sasa Mount Kenya United) msimu huu wa 2018/19, amekuwa na mwanzo mbaya kwenye ligi huku akishinda mechi moja pekee, kusajili sare nne na kupokezwa vichapo viwili kati ya mechi zote saba alizosimamia.

Rais wa Sofapaka Elly Kalekwa aliyetangaza habari hizo, alisema kwamba kocha huyo aliamua kubwaga manyanga baada ya kutotimiza malengo aliyowekewa na usimamizi wa mabingwa hao wa zamani kabla ya mwisho wa msimu.

Kalekwa pia alitangaza kwamba naibu kocha John Baraza ambaye alikuwa mwanasoka veterani wa klabu hiyo na timu ya taifa Harambee Stars miaka ya nyuma atahudumu kama kaimu kocha hadi wapate mrithi wa Medo.

“Ndiyo ni kweli Melis Medo amejiuzulu na si kocha wetu tena. Tuna malengo ya kutimiza msimu huu na pengine baada ya kutapatapa katika mechi za mwanzo ameamua kuagana nasi badala ya kusubiri kuangukiwa na shoka letu. Kwa sasa John Baraza atachukua usukani kama kaimu kocha tukijipanga kutafuta atakayejaza nafasi hiyo,”

“Malengo yetu yanasalia yale yale. Tunataka kushinda ligi msimu huu na hilo bado linawezekana,” akasema Kalekwa.

Hii ina maana kwamba Baraza ambaye pia alihudumu kama kocha wa timu msimu uliopita kabla ya ujio wa Medo atasimamia mechi yake ya kwanza wakati wa pambano la ligi kati ya Sofapaka na SoNy Sugar siku ya Jumamosi Januari 19, 2019.

Raia huyo wa Marekani anaondoka wakati timu hiyo inaendelea kushikilia nafasi isiyo ya kawaida ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la KPL baada ya misururu ya matokeo yasiyoridhisha.

Baadhi ya wanasoka aliowasajili wakati wa kujiunga na Sofapaka ni mamidfilda Tom Adwar, John Avire, Faina Jacobs na Cornelius Juma(wote kutoka Mount Kenya), Cliff Kasuti kutoka Ulinzi Stars, Titus Achesa kutoka Posta Rangers, Richard Aimo aliyekuwa akisakatia Chemelil FC, Ian Wakasala wa Ushuru FC na Ibrahim Kajuba.

You can share this post!

Askofu aombwa akatae gari alilopewa na Ruto

SHAMBULIO: Wanao Khalwale na Mudavadi wanusuriwa

adminleo